Baraka FM
Baraka FM
6 May 2026, 16:37

Kila binadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi duniani ni chache.
Na Hobokela Lwinga
Mwenyekiti mstaafu wa Kanisa la Uinjilisti Tanzania(kwa Lena)Mchungaji Emmanuel Sanga, amefariki dunia alfajiri ya Mei 04,2026 alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Akithibitisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kanisa la Uinjilisti Tanzania, Mchungaji Meshack Ngoni, amesema kifo cha Mchungaji Sanga ni pigo kubwa kwa kanisa hilo, ameeleza kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa waasisi pamoja na mshauri wa kanisa.
Ameongeza kuwa ibada ya mazishi itafanyika katika Kanisa la Uinjilisti Mbalizi kwa Lena, makao makuu ya kanisa hilo, kuanzia saa nne asubuhi, na baadaye maziko yatafanyika nyumbani kwa marehemu,Mbalizi.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamesema watamkumbuka marehemu kwa mchango wake mkubwa wa kiroho, wakimtaja kuwa alikuwa kiunganishi muhimu miongoni mwa waumini.
Kwa upande wake, mtoto wa marehemu, Samwel Sanga, amesema mwili wa baba yao uliwasili nyumbani Mei tano, mwaka huu, na kwamba shughuli za maombolezo zinaendelea nyumbani kwake Mbalizi, eneo la nyuma ya Hoteli ya Tughimbe.
Ameongeza kuwa kabla ya umauti kumfika, marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu.
Marehemu Mchungaji Emmanuel Sanga, baada ya kustaafu, aliendelea kulitumikia kanisa hilo kama mshauri hadi alipofariki dunia.