Baraka FM

Askofu Pangani akemea unyanyapaa kwa wenye mahitaji maalum

19 August 2026, 15:38

Watu wenye mahitaji maalumu ni watu wanaopaswa kutendewa sawa kama ilivyo kwa watu wengine

Na Hobokela Lwinga

Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Robert Yondamu Pangani, ameitaka jamii kuacha unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wenye mahitaji maalumu, badala yake kuwajali, kuwathamini na kuwapatia msaada unaostahili kulingana na mahitaji yao.

‎Askofu Pangani ametoa rai hiyo wakati akifungua Semina ya Udiakonia ya KMT-JKM, iliyowakutanisha taasisi na wadau wa huduma za udiakonia kutoka madhehebu mbalimbali ya dini.

‎Semina hiyo imefadhiliwa na Shirika la Mission 21 na imefanyika katika Makao Makuu ya Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Jakaranda jijini Mbeya.


‎Aidha, Askofu Pangani amesema ni wajibu wa Kanisa kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha watu waliopo katika makundi mbalimbali yenye mahitaji wanapata huduma na msaada unaostahili, ili waweze kuishi maisha yenye utu na usawa katika jamii.

Askofu wa KMT/JKM Robert Pangani(picha na Hobokela Lwinga)
Sauti ya Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Robert Yondamu Pangani


Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Mission 21 nchini Tanzania, Dada Adrian Sweetman, amesema kipaumbele cha shirika hilo ni kuwawezesha watu wenye mahitaji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo afya na uchumi, ili waweze kujitegemea na kuboresha maisha yao.

Sauti ya mwakilishi wa Shirika la Mission 21 nchini Tanzania, Dada Adrian Sweetman



Hata hivyo, Afisa Afya wa Idara ya Udiakonia KMT-JKM, Ndugu Emmanuel Angetile, amewataka watoa huduma kutowabagua wala kuwatenga watu wenye mahitaji maalumu, bali kuhakikisha kila mmoja anapata huduma kwa usawa bila kujali hali yake.

Afisa Afya wa Idara ya Udiakonia KMT-JKM, Ndugu Emmanuel Angetile(picha na Hobokela Lwinga)
Sauti ya Afisa Afya wa Idara ya Udiakonia KMT-JKM, Ndugu Emmanuel Angetile


‎Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Aika Temu, amesema Serikali inalitazama kwa jicho la ziada kundi la watu wenye mahitaji maalumu, wakiwemo watu wenye ulemavu, kwa kuhakikisha wanapatiwa huduma stahiki na kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mbeya Bi. Aika Temu(picha na Hobokela Lwinga)
Sauti ya Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Aika Temu


‎Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wameishukuru Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi kwa kuendelea kutoa huduma na misaada kwa watu wenye mahitaji kupitia Idara yake ya Udiakonia, kwa ufadhili kutoka Shirika la Mission 21.

Washiriki wa semina hiyo(picha na Hobokela Lwinga)
Sauti ya ‎Baadhi ya washiriki wa semina