Baraka FM

Halmashauri ya Songwe yaendelea kuhamasisha mfumo wa stakabadhi ghala kijiji kwa kijiji

3 April 2024, 12:19

Timu maalumu ya mfumo wa stakabadhi ghala inafanya uhamasishaji ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya faida ya mfumo wa stakabadhi ghala ikiwa ni maandalizi ya msimu wa mavuno wa 2023/2024.

Na mwandishi wetu

Timu maalumu ya uhamasishaji wa mfumo wa stakabadhi ghala ya Halmashauri ya Wilaya ya Songwe imeendelea na uhamasishaji wa mfumo huo kijiji kwa kijiji katika halamashauri hiyo.

Timu hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Mheshimiwa Abraham Sambila ambapo imefanya uhamasishaji katika vijiji vya Galula kata ya Galula na Ifwenkenya kata ya Ifwenkenya

Katika uhamasishaji huo,timu hiyo imewahusisha pia Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mhe. Wangala, Mhe Joseph Machimu, Afisa Kilimo, ndugu Anderw Kayombo na Mwanasheria, ndugu Baraka Chaula.

Akizungumza katika katika vijiji hivyo, Mheshimiwa Sambila amewataka wakulima wa ufuta kutumia njia hiyo ya stakadhi ghala katika kuuza ufuta wao kwani mfumo huo umeonekana kuwa na tija kubwa kwa mkulima ukilinganisha na njia ya uuzaji holela kwa walanguzi.

Mwanasheria aliwataka viongozi wa AMCOS kuwa kiungo mhimu cha mfumo huo wa stakabadhi ghala na sio kuwa sehemu ya kuwanyinya wakulima huku akisisitiza kuwa viongozi wa AMCOS watakaobainika kujihusisha na matukio ya kuwaibia au kuwanyonya wakulima watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ilianza mauzo ya zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani msimu wa 2022/2023 ambapo Wilaya hiyo ilipata zaidi ya Sh28 bilioni.

Katika makusanyo hayo zaidi ya Sh26 bilioni zilienda kwa wakulima wa ufuta, zaidi ya Sh800 milioni ikiwa ni mapato ya Halmashauri.