Baraka FM

RC Dendego aingia kazini kusaka mamba Mtera

11 January 2024, 17:46

Na Moses Mbwambo,Iringa

Ikiwa ni siku chache vyombo vya habari kuripoti tukio la mwananchi aliyeliwa na mamba katika bwawa la mtera lililopo kata ya migori, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego leo amefanya ziara katika kata hiyo na kuonana na wananchi na wavuvi wanaovua katika Bwawa hilo.

Awali kabla ya kuzungumza na wananchi hao mkuu wa mkoa alisikiliza maoni yao na kutaka kufahamu nini kifanyike ili kukabiliaba na mamba hao, ambapo wananchi hao walimuomba mkuu wa mkoa kwa kuwa Silaha za kisasa kama Bunduki zinashindwa kufanya kazi majini basi waweze kutumia silaha za asili kama ndoano katika kuwanasa mamba hao ambao wamekuwa na madhara kwa binadamu.

Akizungumza na wananchi hao baada ya kusikiliza maoni yao Mhe. Dendego akatoamaagizo kwa viongozi wa eneo hilo kwa kuwataka kuanza kazi mara moja ya kutega ndoano ili kuwanansa mamba hao pia akawataka TAWA kushirikiana kwa pamoja na viongozi na wananchi katika kila hatua inayofanyika ili kuondokana na changamoto hiyo.

Pia Mhe. Dendego ameongeza kwa kuwaomba wavuvi hao katika kipindi hiki wanapokwenda bwawani kuvua kuhakikisha wananenda kwa makundi ya watu kadhaa na sio kwenda mmoja mmoja ili linapotaka kutokea jambo basi wahakikishe wanakuwa karibu kuweza kusaidiana wakiwa bwawani.

Aidha Mhe. Dendego amesema kuwa katika mwaka wa fedha serikali itatenga fedha kwa wananchi wa kata hiyo kwaajili ya ununzi wa Boti zitakazo wasaidia wavuvi hao katika shuguli zao na kuachana na mitumbwi ambayo kwa sasa inawaletea matatizo pindi wanapofanya shughuli za uvuvi.

Sambamba na hayo wananchi wa kata ya migoli wamemshukuru sana Mkuu wa Mkoa na Serikali kwa kuwatengea fedha kwaajili ya ununuzi wa boti wakisema kuwa uwepo wa boti hizo utauwa ni mkombozi kwao na hakuta kuwa na madhara kama haya.