Baraka FM
Baraka FM
4 April 2025, 20:16

Jeshi la zimamoto limekuwa likitoa elimu ya matumizi ya vifaa vya kuzimia moto pindi unapotokea huku wakisisitiza utoaji wa taarifa mapema yanapotokea majanga hayo.
Na Kelvin Lameck
Moto mkubwa umezuka usiku wa kuamkia leo tarehe 4 April 2025 katika ghala moja la kuhifadhi magodoro lililopo katika mji wa Mbalizi na kusababisha hasara kubwa baada ya magodoro yote kuteketea.
Akizungumza na kituo hiki Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbalizi Paul Komeka Mwampamba amesema chanzo cha moto huo ni mtu mmoja ambaye hajafahamika kwenda kukata kufuli la ghala hilo kwa lengo la kutafuta guta ambalo linadaiwa kuibiwa na kufichwa ndani yake.

Naye Afisa Mtendaji wa kitongoji cha Mbalizi Sumun Malongo amesema baada ya jeshi la zimamoto kufanikiwa kuzima moto huo ndani hawakuona guta lolote jambo ambalo limesababisha usumbufu kwa wananchi ili hali watu waliokuwa na nia ya kutafuta guta hilo hawakutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa.

Kwa upande wake kamanda wa polisi wa jeshi la zima moto na uokoaji mkoa wa Mbeya Malumbo Ngata amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo wamefika eneo la tukio na kufanikiwa kudhibiti moto huku akiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa mapema.
Kamanda Ngata amesema mpaka sasa thamani ya mali iliyoharibika bado haijajulikana na hakuna madhara ya kibinadamu yaliyotokea hivyo wanaendelea na uchunguzi na utakapokamilika watatoa taarifa kamili.

Aidha Mfanyabiashara wa magodoro Hagai Mwaisanila amesema ndani ya Godown hakukuwa na Guta hivyo amewaomba viongozi wa mtaa huo kuweka ulinzi kwenye eneo hilo ili kusitokee udanganyifu wa aina yoyote.