Mazingira FM

Ashikwa na mamba akiwa kwenye mtumbwi wakati akiendelea na shughuli za uvuvi.

19 February 2023, 9:07 pm

Mayela Maleba (37) Mkazi wa Tamau kata ya Nyatwali Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara amekamatwa na mamba wakati akiendelea na shughuli za uvuvi wa samaki kandokando ya ziwa Victoria eneo la Tamau.

Mwanamme huyo ambaye mpaka sasa bado hajapatikana amekamatwa leo jumapili tarehe 19 Feb 2023 majira ya saa 3:00 asubuhi wakati akiwa anavua samaki katika mpaka wa eneo la mtaa wa Tamau na Nyatwali akiwa kwenye mtumbwi mdogo maarufu kama denge ambapo juhudi za wananchi waliokusanyika kwa ajili ya kumtafuta bado hazijafanikiwa kumpata.

Mashuhuda wa tukio hilo wakizungumza na Radio Mazingira Fm kwa nyakati tofauti wamesema walisikia sauti ya mtu anapiga kelele kuomba msaada na waliposogea katika eneo la tukio walimuona mtu huyo akiwa amepanda katika matete yaliyokuwa yakielea ndani ya maji na baada ya sekunde chache mamba alimrukia na kuzama naye.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio la mamba

Kufuatia tukio hilo Katibu Tawala Wilaya ya Bunda DAS, Salumu Mtelela amefika eneo la tukio na kuwapa pole wakazi hao na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhali wanapokwenda ziwani kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Salum Mtelela katibu tawala wilaya ya Bunda akizungumza na wakaazi wa kata ya nytatwali wakati wa zoezi la utafutaji wa mwananchi aliyekamatwa na Mamba