Mazingira FM

Bunda: Upungufu wa matundu ya vyoo, madarasa na wazazi kushindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao bado ni changamoto ya elimu kata ya Kabarimu.

11 February 2023, 6:52 pm

Afisa Elimu kata ya Kabarimu, Tabu Hamis Omary

Uongozi wa Kata ya Kabarimu Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara umefanya hafla fupi ya kuwapongeza walimu wa kata hiyo kwa kuonesha bidii kubwa katika ufundishaji unaoleta matokeo chanya kwa wanafunzi wao.

Hafla hiyo fupi imefanyika jana tarehe 10 Feb 2023 katika ukumbi wa shule ya sekondari Bunda ikiwahusisha viongozi wa kata hiyo wakiongozwa na diwani, Afisa Elimu Kata, wakuu wa shule na walimu wote wa kata hiyo.

Awali akisoma Risala mbele ya Mgeni rasmi, Afisa Elimu kata ya Kabarimu, Tabu Hamis Omary amesema taaluma itolewayo katika shule za kata hiyo imekuwa ikii hadi siku licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa ambazo nyingine zipo nje ya uwezo wao

Aidha katika risala hiyo Bi Tabu Omary amezitaja changamoto mbalimbali zinazowakabiri ikiwa ni pamoja na upungufu wa mabweni ya wanafunzi shule ya sekondari Bunda, upungufu wa madarasa kwa shule za msingi, upungufu wa matundu ya vyoo kwa shule zote na wazazi kushindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao.
Mwenyekiti wa wazazi CCM wilaya ya Bunda, Leonard Elias Magwayega

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mwanasheria wa Kijitegemea ambaye pia ni Mwenyekiti wa wazazi CCM wilaya ya Bunda, Leonard Elias Magwayega amesema changamoto hizo zitaondoka kwa kuweka ushirikiano

By Edward Lucas