Baraka FM

Askofu Pangani:Maombi ni msingi wa kutatua changamoto za taifa na kanisa

7 April 2026, 09:21

Askofu Robert Pangani akitoa mbaraka wa kufunga Ibada ya pasaka katika kanisa Moravian ushirika wa Songwe Viwandani (picha na Hobokela Lwinga)

Jukumu la kanisa ni kuombea amani ya taifa,kwani maombi yana nguvu ya kuleta utulivu,umoja na mshikamano hivyo huchangia maendeleo endelevu ya jamii na nchi kwa ujumla.

‎Na Hobokela Lwinga

‎Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi, Robert Pangani, amesema kuwa maombi ni nguzo muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili viongozi, taifa pamoja na kanisa kwa ujumla.

‎Askofu Pangani ametoa kauli hiyo wakati wa ibada ya Jumapili ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Moravian Tanzania, Ushirika wa Songwe Viwandani, uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Askofu kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi Robert Pangani (picha na Hobokela Lwinga)

‎Amesema kuwa hakuna suluhu ya kudumu ya matatizo ya jamii pasipo kumtegemea Mungu kupitia maombi, huku akilihimiza kanisa kuendelea kuliombea taifa ili liendelee kuwa na amani na utulivu.

Baadhi ya waumini katika Ibada ya pasaka katika ushirika wa Songwe Viwandani (picha na Hobokela Lwinga)


‎Aidha, ameonya kuhusu athari za vita vinavyoendelea katika baadhi ya mataifa duniani, akieleza kuwa machafuko hayo yanaathiri pia uchumi wa nchi nyingine, ikiwemo kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama mafuta.

Askofu Pangani akiwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza la wazee wa ushirika wa Songwe Viwandani(picha na Hobokela Lwinga)


‎Katika hatua nyingine, Askofu Pangani ametoa wito kwa jamii kuhubiri amani kuanzia ngazi ya familia hadi taifa, akisisitiza kuwa kila mmoja ana jukumu la kudumisha amani katika eneo lake.

Askofu Robert Pangani (kulia)akiwa na mchungaji wa Ushirika wa Songwe mchungaji Israel Isote.


‎Pia amewahimiza wazazi kuwalea watoto katika misingi bora kwa kuwapa elimu sahihi, ili waweze kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Askofu Robert Pangani(katikati) akisalimiana na watoto wa shule ya jumapiili (kulia)ni mke wa askofu mch.Bahati Mshani(kushoto)ni mchungaji wa Ushirika wa Songwe Viwandani Israel Isote.

Katika ibada hiyo, huduma mbalimbali zilifanyika kwa utaratibu mzuri, zikiwemo huduma za kurudi kundini,ubatizo wa watoto,pamoja na kujiunga na Kanisa.

Askofu Robert Pangani akiwa amembeba mmoja wa mtoto aliyembatiza(picha na Hobokela Lwinga)