Baraka FM
Baraka FM
22 February 2026, 13:19

Kitabu cha Kutoka 20:24–26, ambapo Mungu alimwagiza Musa awajulishe Waisraeli wamjengee madhabahu ya udongo au mawe yasiyochongwa, na wasitumie ngazi kupanda juu yake,akiwa na Maana kwamba ibada ilipaswa kufanywa kwa unyenyekevu na usafi wa moyo, Hivyo, ujenzi wake ulionyesha kuwa uhusiano na Mungu haujengwi kwa fahari ya nje bali kwa utiifu na moyo wa kweli.
Na Hobokela Lwinga
Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi, Mch. Lawrence Nzowa, amewataka Wakristo kuwa na moyo wa ukarimu kwa wachungaji na makuhani wanaohudumu katika sharika zao ili kuunga mkono kazi ya Mungu wanayoifanya.
Rai hiyo ameitoa katika salamu zake wakati wa ibada ya Jumapili iliyofanyika tarehe 22 Februari 2026 katika Ushirika wa Vwawa, Jimbo la Mbozi mkoani Songwe.

Katika ibada hiyo, Mch. Nzowa alimpongeza mchungaji wa Ushirika wa Vwawa kwa usimamizi mzuri wa jengo la kuabudia, akieleza kuwa juhudi hizo zinachangia kukuza na kuimarisha huduma ndani ya kanisa.
Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na kwaya ya vijana wa zamani kutoka Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, ambao walitoa zawadi mbalimbali kwa wanawake wazee, wachungaji wastaafu, na pia kuuchangia ushirika huo kiasi cha shilingi laki tano kwa ajili ya ujenzi wa kanisa.

Aidha, Wakristo walioshiriki ibada hiyo walitoa sadaka zao katika hafla fupi ya uzinduzi wa sadaka ya ujenzi wa jengo la kuabudia katika Ushirika wa Vwawa.
Akihitimisha ibada hiyo, Mchungaji wa Ushirika wa Vwawa, Mch. Anania Tweve, aliwashukuru Wakristo wote kwa moyo wao wa kujitolea na kwa sadaka walizotoa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kanisa.
