Baraka FM
Baraka FM
19 February 2026, 18:28

Mahakama kuu ya Tanzania yatambua mchango wa taasisi ya baraka media tanzania kwa kuitunuku tuzo ya umahili wa utengenezaji wa maudhui.
Na Hobokela Lwinga
Taasisi ya Baraka Media Tanzania, inayomiliki Baraka FM Radio na Baraka TV, imeishukuru Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kuitunuku tuzo ya kutambua ushirikiano wake katika kuandaa na kurusha vipindi mbalimbali vinavyohusu masuala ya mahakama na utoaji wa haki kwa jamii.

Shukrani hizo zimetolewa na Meneja wa Baraka FM Radio, ndugu Charles Amlike, mara baada ya kupokea tuzo hiyo iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya. Tuzo hiyo ilikabidhiwa katika maadhimisho ya Siku ya Mahakama yaliyofanyika Februari 02, 2026, jijini Mbeya.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Amlike amesema kuwa ushirikiano kati ya vyombo vya habari na taasisi za umma ni muhimu katika kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya kisheria na haki zao za msingi. Ameeleza kuwa Baraka Media itaendelea kutoa nafasi kwa mahakama na taasisi nyingine kufikisha ujumbe kwa jamii kwa njia sahihi na yenye tija.

Katika hatua nyingine, ameziomba taasisi mbalimbali za umma na binafsi kutumia jukwaa la Baraka Media katika kuelimisha jamii kwa mawanda mapana zaidi, akisisitiza kuwa chombo hicho kiko tayari kushirikiana na wadau wote kwa lengo la kujenga jamii yenye uelewa na maendeleo.
Baadhi ya watangazaji wa Baraka FM wamesema tuzo hiyo ni chachu ya kuongeza bidii na weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Wameahidi kuendelea kushirikiana vyema na taasisi zote zinazohitaji kushirikiana nao katika kutengeneza na kurusha maudhui yenye manufaa kwa jamii.
