Baraka FM

Baraka FM yapewa tuzo utengenezaji maudhui ya mahakama

19 February 2026, 08:46

Tuzo iliyotolewa na Mahakama Kuu kwa kituo cha utangazaji cha Baraka FM (picha na Hobokela Lwinga)

Kwa muda mrefu Baraka fM imekuwa ikitoa vipindi na taarifa mbalimbali zinazolenga kuelimisha jamii kuhusu sheria, taratibu za kimahakama na utoaji wa haki, hivyo kusaidia kuongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na vyombo vya habari.

‎Na Hobokela Lwinga

Baraka FM Radio, iliyo chini ya taasisi ya Baraka Media Tanzania, imepokea tuzo maalum ya kutambua ushirikiano wake mkubwa inaoutoa kwa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Yuda Jay, miongoni mwa watangazaji katika kipindi cha Muda Wetu katika Baraka FM radio akiwa na tuzo wakati akiendelea na kipindi hicho (picha na Hobokela Lwinga)

Tuzo hiyo ni ishara ya kuthamini mchango wa chombo hicho cha habari katika kuhabarisha umma kuhusu masuala ya mahakama na utoaji wa haki.

‎Tuzo hiyo imetolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mahakama yaliyofanyika Februari 2, 2026.

‎Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya mahakama hiyo mkoani Mbeya, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, mahakama pamoja na wadau wa sekta ya mahakama.

‎Kupitia tuzo hiyo, Mahakama Kuu imetambua mchango wa Baraka FM katika kusambaza taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu shughuli za mahakama, hatua zinazochukuliwa katika utoaji wa haki, pamoja na elimu ya sheria kwa jamii.

‎Kwa muda mrefu, Baraka Media Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na watumishi wa Mahakama Kuu kwa kuandaa na kurusha vipindi maalum vinavyolenga kutoa elimu kwa umma, Vipindi hivyo vimekuwa vikigusia masuala mbalimbali ya kisheria, haki za raia, na taratibu za kimahakama.

‎Ushirikiano huo umechangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mifumo ya utoaji haki nchini na kuimarisha uwazi kati ya Mahakama na jamii.

‎Kupokea tuzo hii ni hatua nyingine muhimu inayoonesha dhamira ya Baraka Media Tanzania katika kuendelea kuhabarisha na kuelimisha umma kwa weledi na uwajibikaji.