Baraka FM

Mwalimu afia ndani ya nyumba, mwili wake waharibika vibaya

16 January 2026, 09:37

Mwili wa marehemu Zainabu Mwalyepelo ukichukuliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya uchunguzi

Mwili wa marehemu Zainabu Mwalyepelo umechukuliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya kukutwa ndani akiwa amefariki wiki tatu zilizopita.

Na Ezekiel Kamanga

Simanzi zimetawala kwa wakazi wa Mtaa wa Igodima Kata ya Iganzo Jijini Mbeya baada ya mwili wa Mwalimu shule ya sekondari Itiji Zainabu Mwalyepelo ambaye pia ni mwanachuo wa CUoM Mbeya mwili wake kukutwa amefariki nyumbani kwake baada ya kutoonekana kwa zaidi ya wiki tatu bila mafanikio.

Baba Mzazi wa Mwalimu Zainabu Mwalyepelo Mzee Jacob Mwalyepelo amesema mwishoni mwa mwaka jana mwanawe alikuwa amelazwa katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa maradhi ya moyo baada ya matibabu alirejea nyumbani kwake ambako alikuwa akiishi peke yake.

Kutokana na hali ya ugonjwa Baba Mzazi alimshauri Mwalimu aende kujitazamia kwa Dada yake eneo la Ituha lakini marehemu alikataa kwa kuwa alikuwa na maandalizi ya mitihani.

Marehemu Zainabu Mwalyepelo enzi za uhai wake

“Baada ya ukimya wa muda mrefu nilimpigia simu ili kumjulia hali lakini simu haikupokelewa,ndipo januari 13,2026 nilitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa na baadae Polisi.

Mzee Jacob Mwalyepelo anaeleza kuwa baada ya taarifa ya Mwenyekiti na Jeshi la Polisi walitoa kibali nyumba ya mwalimu huyo aliyokuwa akiishi peke yake kuvunjwa hatimaye mwili wake kukutwa kwenye kiti ukiwa umeharibika vibaya.

Baadhi ya wananchi wakiwa eneo la tukio

Ayub Mwazyele Mwenyekiti wa Mtaa wa Igodima Kata ya Iganzo Jijini Mbeya anaeleza kuwa alipokea taarifa za tukio hilo na hatua alizozichukua ni pamoja na kushirikiana na ndugu kuvunja mlango walikuta mwili wa marehemu kwenye kiti ukiwa umeharibika vibaya.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Igodima Kata ya Iganzo Jijini Mbeya Ayub Mwazyele

Majirani wa mtaa huo akiwemo Herman Kanjanja wanaeleza namna jirani yao alivyokuwa akiishi na hofu yao kutanda baada ya ukimya na kutoonekana kwake kwa muda mrefu kutokana na tabia ya Mwalimu kuwa akipiga ngoma na kuimba mara kwa mara.