Baraka FM
Baraka FM
25 September 2025, 15:50

Kusaidia watu wenye mahitaji ni sehemu ya maagizo ya Mungu kwenye maandiko Matakatifu yaani Biblia Yakobo 1:27 inasema “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.”
Na Hobokela Lwinga
Viongozi wa udiakonia wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi wametakiwa kufanya kazi ya udiakonia kwa weledi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii na kusaidia makundi ya watu wasiojiweza.
Rai hiyo imetolewa na mkufunzi wa semina za Udiakonia Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini Lulu Mpenja wakati akifundisha semina ya udiakonia kwa viongozi wa udiakonia wilaya ya Mbalizi iliyofanyika katika ushirika wa Mlima reli.
Katika hatua nyingine mkufunzi huyo amesema wajibu wa mdiakonia ni kuwezesha kuwajengea uwezo watu wenye uhitaji mbalimbali namna ya kujitegemea katika maisha yao.

Akifundisha somo la upimaji wa VVU na faida zake Juliana Willa amewakumbusha washiriki kutokuwanyanyapa wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi huku akitaja faida ya kupima kuwa ni kujua afya yako na namna ya kuishi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kanisa la Moravian Tanzania wilaya ya Mbalizi mch.Erica Mwanijembe amewataka viongozi hao kutumia nafasi ya elimu waliyoipata kuhamasisha wakristo kwenye shirika zao kushiriki vyema kushiriki sikukuu ya udiakonia inayotarajia kufanyika October 12,mwaka huu.

Baadhi ya washiriki wamelishukru kanisa kupitia idara ya udiakonia kwa kuendelea kutoa elimu ambayo inawawezesha kufanya kazi yao ya udiakonia kwa weledi.

Ikumbukwe kuwa semina zote zinatolewa na idara ya udiakonia katika Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi zinafadhiliwa na shirika la mission 21.