Baraka FM

Mahakama yatupilia mbali kesi ya mke wa Mdude dhidi ya IGP na wengine

10 July 2025, 13:27

Ndani ya Chumba cha mahakama wananchi na wakili wa utetezi na serikali wakiwa wanasubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi(picha na Ezekiel Kamanga)

Ni miezi kadhaa sasa tangu kada wa CHADEMA Mpaluka Nyagali maarufu kwa jina la Mdude achukuliwe na watu wasiojulikana nyumbani kwake Iwambi jijini Mbeya.

Na Ezekiel Kamanga

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imetupilia mbali maombi ya jinai namba 14538/2025 yaliyofunguliwa mei 17,2025 na Sije Mbughi mke wa Mpaluka Nyagali(Mdude) dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP), Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa mashitaka(DPP),Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya(RPC), Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mbeya(RCO) na askari Shaban Charo anayedaiwa kuwa ndiye aliyemchukua Mdude ambapo maombi yameanza kusikilizwa juni 30,2025 na kutolewa uamuzi Julai 9,2025 na Jaji Said Kalunde.

Mleta maombi Sije Mbughi amewakilishwa na Wakili Bonifase Mwabukusi, Wakili Hekima Mwasipuy na Wakili Solomon Kamunyu ambapo upande wa wajibu maombi umewakilishwa na Wakili Domick Mushi pamoja na Wakili Adalbert Zegge huku Sije akitaka mumewe kufikishwa mahakamani na kufungulia mashitaka kwa mujibu wa sheria.

Jaji Said Kalunde ameanza kutoa uamuzi majira ya saa 9:35 alasiri na kuhitimishwa saa 11:50 jioni awali Jaji Said Kalunde amesema upande wa mleta maombi akiwemo Sije Mbughi na Ezekiel Sheyo.

Upande wa waleta maombi kupitia Ezekiel Sheyo umedai alipigiwa simu na Shaban Charo siku mbili kabla ya tukio hilo liliotokea mei 2,2025 Kata ya Iwambi Jijini Mbeya ambapo mkewe alidai askari Shaban Charo akiwa na askari wengine wakiwa na bunduki mbili na nyundo walimpiga kwa nyundo kichwani kisha kuvuja damu na kumburuza nje na hajaonekana mpaka sasa.

Ezekiel Sheyo amesema alikataa kuonesha nyumbani kwa Mdude licha ya kubughudhiwa mara kwa mara na Shaban Charo hivyo kuamua kutoa taarifa kwa kiongozi wa CHADEMA China wa China lakini alishangazwa na kupata taarifa za Mdude kuvamiwa na kupigwa.

Aidha mke wa Mdude ameshindwa kuanisha namba za askari Shaban Charo ilhali alishindwa kuunganisha maelekezo ya Ezekiel Sheyo kwani Sheyo hakutoa taarifa kwa Sije Ili kumtahadhatisha uvamizi uliotatarajiwa kufanywa.

Kwa upande wa wajibu maombi Jaji Said Kalunde amesema hoja zao za kupinga wajibu maombi kuhusika na tukio la utekaji kwani walipaswa kuleta ushahidi wa utambuzi akiwemo askari Shaban Charo na Kituo chake cha kazi pamoja na Kituo alichopelekwa Mdude.

Baada ya kuzisikiliza hoja za upande wa waleta maombi na wajibu maombi Jaji Said Kalunde amesema hoja zote zina mashiko akianza na upande wa waleta maombi wakiongozwa na Wakili Bonifase Mwabukusi hasa pale aliposema kila binadamu ana haki zake za msingi ikiwemo ya kuishi.

Malunde amesema upande wa waleta maombi umeshindwa kuthibitishwa wahusika wa tukio hilo kwa utambuzi wa aina yoyote.

Kabla ya kutoa uamuzi Jaji Said Kalunde ametoa ushauri kwa mwendesha mashitaka na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa makosa mbalimbali yakiwemo ya utekelezaji ambayo yamekuwa yakilalanikiwa.

Kalunde amesema hoja ya Sije Mbughi haikusikilizwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya badala yake ikatolewa taarifa na Jeshi la Polisi kuwa suala hilo linafanyiwa uchunguzi na baada ya kutopewa majibu ikamlazimu kwenda mahakamani ili kupata ufumbuzi.

Hata hivyo ameshauri mwendesha mashitaka na Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi wa makosa mbalimbali ili kuondoa malalamiko kwenye jamii.

Akitoa uamuzi wa maombi hayo Jaji Said Kalunde amesema hoja zilizoletwa na waleta maombi hazina mashiko kwa kuwa wameshindwa kuthibitisha kwa vielelezo.

Nje ya Mahakama Wakili Bonifase Mwabukusi ameupokea uamuzi wa Mahakama hivyo watapata mchanganuo wake kwa kushirikiana na Mawakili wenzaji kuona hatua watakazozichukua ikiwemo kupeleka Mahakama za kimataifa na isionekane hawana uzalendo bali wanaitafuta haki ya Mdude.

Sauti ya Wakili Bonifase Mwabukusi

Naye Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Frank Mwakajoka amesema wanafungua kesi nyingine kwa ajili ya Dionis Kipanya ambaye anadaiwa kutekwa.

Sauti ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Frank Mwakajoka

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya Masaga Kaloli amewataka wanachama kuendelea kushikamana na wapo tayari kushiriki mchakato wa kuchangia familia ya Mdude.

Sauti ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya Masaga Kaloli