Baraka FM

Wawili wanusurika kifo baada ya magari kugongana na kuwaka moto Mbeya

14 March 2025, 08:08

Muonekano wa magari baada moto kuzimwa eneo la tukio (picha na na Ezekiel Kamanga)

Elimu ya udereva imekuwa ikiwasisitiza madereva kuwa makini natika uendeshaji wao wa vyombo vya moto,licha ya hivyo madereva wengi wamekuwa wakiukwaji wa sheria na taratibu za barabara.

Na Ezekiel Kamanga

Watu wawili wamenusurika kifo baada ya ajali ya magari mawili kugongana kisha kuwaka moto eneo la Kijiji cha Majombe Kata ya Itamboleo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya majira ya saa 2:55 usiku machi 12,2025.

Akitoa taarifa kwa Wanahabari Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya Malumbo Ngata amesema walipata taarifa kutoka kwa Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia(FFU) Koplo Jiles Simwandu ikieleza magari kugongana ndipo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liliondoka haraka kuelekea eneo la tukio umbali wa kilometa mia moja arobaini kutoka Jijini Mbeya.

Malumbo Ngata ameyataja magari mawili yaliyogogana kisha kuwaka moto ni aina ya Scania yenye namba za usajili T 326 AUD likiendeshwa na dereva Ahazi Mwasanga likitokea Dar es Salaam kuelekea Kyela na T 297 CZS likitokea Zambia kwenda Jijini Dar es Salaam ambalo dereva wake hakujulikana mara moja.

Jitihada za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifanikiwa kuudhibiti moto huo na kuokoa baadhi ya mali zilizokuwemo kwenye magari hayo na hakukuwa na kifo chochote.Waliojeruhiwa ni pamoja na Ahazi Mwasanga(29) na Saviola Ngaa Rashid(21).

Kamanda amesema hasara iliyopatikana ni pamoja na kuungua cabin namba T 297 CZS na T 326 AUD iliyoteketea yote Aidha Malumbo Ngata amebainisha chanzo cha ajali ni dereva wa gari namba T CZS kushindwa kulimudu gari lake na kusababisha kugongana na gari T 326 AUD na kusababisha kuzuka kwa moto.

Kamanda Malumbo amewataka madereva kuwa makini wawapo barabara sanjari na kuhakikisha magari yao kuwa na vizimia moto(Fire Extinguisher)ili moto usilete madhara makubwa.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kuitumia kikamilifu namba 114 ya dharula ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Ili kuwahi kwa wakati pindi yanapotokea majanga yakiwemo ya ajali za barabarani, mgodini,kuzama majini,visimani na ajali za moto.