

13 March 2025, 22:21
Viongozi wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi wametembelea taasisi za kanisa zinazomilikiwa na jimbo kwa lengo la kushauriana namna bora ya kuimarisha utendaji kazi.
Na Hobokela Lwinga
Watumishi wanaofanya kazi katika taasisi mbalimbali za kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kusini Magharibi wametakiwa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kuhakikisha taasisi hizo zinafanya vizuri.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti na Kaimu Katibu Mkuu wa kanisa hilo Jimbo la Kusini Magharibi Mch. Asulumenye Mwahalende wakati wa ziara yao leo kwenye kituo cha Redio Baraka.
Mchungaji Mwahalende amewataka watumishi wa taasisi hiyo kufuata majira ya kanisa katika vipindi vyake ikiwa ni pamoja na kuhimiza wakristo kutambua umuhimu wa mwezi wa kwaresma unaoendelea sasa.
Kwa upande wake Mkaguzi wa ndani Ndugu Jail Mwasegile ameitaka taasisi ya Redio Baraka kuzingatia utunzaji wa mali ya kanisa pamoja na maboresho ya idara za fedha.
Hata hivyo Mkurugenzi wa rasilimali watu na mwanasheria wa Jimbo Mch. Nsevilwe Msyaliha amesema ni vizuri watumishi kutambua utendaji wao wa kazi kwa kufuata sheria na miongozo ya ajira ya kazi.
Miongoni mwa taasisi zilizotembelewa na viongozi hao ni pamoja na taasisi ya chuo cha ufundi Moravian, taasisi ya redio Baraka na chuo Mbeya Moravian teachers college zote zinapatikana jijini Mbeya.