Ujerumani, kanisa la Moravian kushirikiana kutekeleza miradi ya maendeleo
2 December 2024, 14:17
Ushirikiano ni jambo zuri ambalo linaleta matokeo chanya na ili uweze kufanikiwa unapaswa kuwa na ushirikiano na wengine,wanasema “kidole kimoja hakivunji chawa.”
Na Kelvin Lameck
Uongozi wa Kanisa la Moraviani Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi umesema utaendelea kusimamia kwa uaminifu fedha zinazotolewa na wafadhili wake kutoka nchini ujerumani ili zitumika kama zilivyopangwa.
Hayo yamesemwa na Katibu mkuu wa kanisa hilo jimbo la kusini Magharibi Israel Mwakilasa baada ya wafadhili hao kufanya ziara katika chuo cha ufundi Moraviani kilichopo kadege jijini Mbeya.
Mwakilasa amesema lengo la ziara ya wageni hao ni kujionea namna miradi mbalimbali inavyotekelezwa chuoni hapo ikiwemo ujenzi wa njia ya kupita walemavu,mradi wa maji safi na salama na ujenzi wa jengo la maonesho mambo mbalimbali yanayofanyika chuoni hapo.
Aidha amewataka waumini wa kanisa la Moraviani kujitokeza kwa wingi kesho kupiga kura kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa kanisa hilo Asulumenye Mwahalende amesema amewashukru wafadhili hao kwa kuwa wamekuwa msaada mkubwa kwa kutoa fedha zinazosaidia uendeshaji wa chuo cha ufundi Moraviani.
Hata hivyo Mkuu wa chuo hicho Erick Mwakasege amesema watahakikisha wanashirikiana na kanisa ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuanza kufanya kazi.