Baraka FM

Wabaptist Mbeya waingia kuombea amani chaguzi 2024/2025

15 October 2024, 19:26

Baadhi ya washiriki katika ibada ya maombi(picha na Josea Sinkala)

Wakristo wametakiwa kuwa mastari wa mbele kuendelea kuliombea taifa hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi.

Na Josea Sinkala

Kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji nchini Tanzania, wachungaji na waumini mbalimbali jijini Mbeya wamejitokeza kwenye maombi ya kuliombea Taifa ikiwemo kukemea roho za utekaji na mauaji.

Ibada ya maombi hayo imefanyika katika kanisa la Baptist Ilomba jijini Mbeya ambapo askofu wa kanisa hilo jimbo la Mbeya Mchungaji Patrick Mwalusamba, amesema ni vizuri waumini na wachungaji wakajifunza kuomba na kusikiliza kwasababu Mungu anasema.

Askofu Mwalusamba, amesema Taifa (Tanzania) linaghubikwa na matukio mbalimbali yanayohitaji msaada wa Mungu mwenyewe ikiwemo chaguzi, kuombea amani na kukataa roho ya utekaji na mauaji.

“Kuna mambo kama ya utekaji ni mambo mabaya lazima kanisa tuingie kuomba na tusikilize, yamkini Mungu akasema acheni kitu fulani au fanyeni hivi na hivi ili tuwe salama kwahiyo ni muhimu tuombe lakini pia tusikilize sauti ya Mungu kama Biblia inavyosema mkijinyenyekeza na Miata njia zenu mbaya yeye Mungu mbinguni atasikia na atatujibu”, amesema askofu Patrick Mwalusamba.

Katika mahojiano yake na kituo hiki baada ya maombi hayo, amesema kuhusu mwalimu Nyerere kwamba “Hayati mwalimu Julius Nyerere binafsi na kwa mtazamo wangu namkumbuka kwa kufanya Taifa kutokuwa la kikabila na misingi ya kuabudu haijayumba. Yaani leo hii mfano hata kwenye uchaguzi tutachagua viongozi bila kujali dini ya mtu”, amesema Mwalusamba.

Askofu wa kanisa la Baptist jimbo la Mbeya Mchungaji Patrick Mwalusamba(picha na Josea Sinkala)

Kwa upande wake Mchungaji Green Ngusa wa kanisa la Baptist Ilomba amesema Taifa linapoangukia kwenye mambo mabaya ikiwemo mauaji ni lazima kanisa liingie kwenye maombi na kukemea maovu ndani na nje ya kanisa.

Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Morris Malisa ameshiriki maombi hayo na kuwaomba viongozi wa dini na waumini kwa ujumla kuendelea kuliombea Taifa na kuwa raia wema kwa maendeleo ya Taifa.

Amewataka pia kuendelea kujiandikisha kwenye daftari la mkazi la mpiga kura ili kuchagua viongozi wanaowataka.

Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Morris Malisa(picha na Josea Sinkala)

Baadhi ya waumini walioshiriki ibada hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mbeya wamesema wana imani Mungu atawasaidia kuwa na Taifa lenye amani na utulivu, kukoma matukio ya mauaji, ukatili na utekaji pamoja na kupata viongozi bora kwenye chaguzi zijazo.

Maombi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiroho kutoka jiji la Mbeya na nje ya jiji pia kwa ajili ya kuliombea Taifa la Tanzania juu ya amani ya nchi, kukemea uovu ndani ya nchi, kuombea chaguzi zijazo pamoja na kuombea Taifa teule la Israel.

Baadhi ya viongozi na wachungaji wa madhehebu ya dini walioshiriki shiriki maombi hayo(picha na Josea Sinkala)