Moto waunguza bweni, wanafunzi 107 wakosa pa kulala Mbeya
26 August 2024, 17:44
Katika hali ya kusikistisha moto umezuka katika bweni la wanafunzi na kusababisha kukosa pa kulala.
Na Hobokela Lwinga
Wanafunzi 107 wa Shule ya Sekondari Nsenga, jijijini Mbeya wamenusurika kifo baada ya bweni walilokuwa wakilala kuwaka moto huku vitu vyote vikiteketea.
Katika tukio hilo lililotokea leo Jumatatu Agosti 26, 2024 saa 5 asubuhi, wanafunzi wanane wamepatwa na mshtuko na wamepelekwa hospitali kupatiwa huduma zaidi.
Akizungumza shuleni hapo, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Malumbo Ngata amesema pamoja na moto huo kutokuwa na athari ya kibinadamu, umeteketeza mali kwa asilimia kubwa.
Amesema tukio hilo limetokea asubuhi wakati wanafunzi wakiwa darasani wakiendelea na masomo na kufanya mali zilizokuwa ndani kuteketea.
“Tulipopata taarifa Jeshi la Zimamoto lilifika haraka eneo la tukio na tulifanikiwa kuuzima moto, japokuwa mali zilizokuwamo kwa kiasi kikubwa zimeteketea. Tunashukuru hakuna mwanafunzi aliyepoteza uhai.
“Bweni lilikuwa na jumla ya wanafunzi 107. Ni wanafunzi wanane pekee walipata mshituko kutokana na tukio hilo, ila afya zao zinaendelea vizuri. Bado chanzo hakijafahamika na tunaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine” amesema Ngata.