Wakristo Mbeya wafanya maombi maeneo ya ajali zinakotokea mara kwa mara
14 July 2024, 11:37
Kutokana na ajali za mara kwa mara mkoani Mbeya zimewafanya wakristo kufanya ibada ya maombezi kukomesha matukio hayo.
Na Deus Mellah
Jukwaa la wakristo wa madhehebu mbalimbali mkoani Mbeya wamefanya maandamano ya amani na kuombea maeneo ambayo ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuombea eneo la mteremko wa mlima Iwambi na mteremko wa Mbembela.
Baada ya maombi hayo kufanyika ibada ilihitimishwa katika kanisa la Moravian jimbo la Kusini Magharibi ushirika wa Iyunga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali.
Akizungumza katika tukio hilo askofu wa kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kusini Magharibi Mch Robert Pangani ameishukuru serikali kwa kuwaunga mkono katika tukio hilo huku akiwaasa wakristo kuendelea kuiunga mkono serikali katika shughuli mbalimbali za maaendeleo.
Askofu Robert Pangani amewaomba wakristo kuendelea kuombea majanga mbalimbali yasiendelee kutokea nchini yakiwemo mauaji ya watu wenye ulemavu, unyanyasaji na mmomonyoko wa maadili.
Aidha mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa mbeya ambaye ni mkuu wa wilaya ya chunya kamishina msaidizi wa jeshi la uhamiaji Mbaraka Batenga amelishukuru jukwaa hilo la wakristo kwa kuona umhimu wa kuombea mkoa na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya sanjari na hayo mch Osia Mbotwa mwenyekiti wa kanisa la Moravian wilaya ya Mbeya akimwakilisha mwenyekiti wa jukwa la wakristo mkoa wa Mbeya amesema lengo la maombi hayo ni kuomba kwa Mungu ili kuondoa ajali za mara kwa mara mkoani humo.
Nao baadhi ya wachungaji na wakristo walioshiriki katika maombi hayo wameomba maombi hayo yawe endelevu.