Baraka FM

Askofu Pangani ashiriki semina ya wachungaji Moravian Chunya

13 March 2026, 17:54

Askofu kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi Robert Pangani (kushoto)akisalimiana na mwenyekiti kanisa la Moravian wilaya ya Chunya mch.Nuru Mwamahonje(kulia)

Semina hiyo imeelezwa kuwa sehemu muhimu ya kuendelea kuimarisha utendaji wa kazi za kiroho katika Kanisa la Moravian, kwa lengo la kulijenga kanisa imara na lenye kuendelea kukua kiroho.

Na Hobokela Lwinga

Wilaya ya Chunya ya Kanisa la Moravian mapema leo imefanya semina maalum kwa wachungaji na wainjilisti wanaohudumu katika wilaya hiyo.

Semina hiyo imefanyika katika Kanisa la Moravian ushirika wa Kibaoni,Lengo la semina hiyo ni likiwa kuwajengea uwezo watumishi hao wa Mungu ili kuimarisha huduma zao na kuongeza ufanisi katika kazi ya kuhubiri Injili.

Semina hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, akiwemo Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania – Jimbo la Kusini Magharibi, Askofu Robert Pangani, Makamu Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania – Jimbo la Kusini Magharibi, Mchungaji Agnes Njeyo, Mwenyekiti wa Wilaya ya Chunya ambaye pia ni mwenyeji wa semina hiyo, Mchungaji Nuru Mwamahonje, pamoja na Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbalizi, Mchungaji Robert Sikanyika.

Aidha, katika semina hiyo wachungaji na wainjilisti wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu wa utumishi wao kutoka katika maeneo mbalimbali wanakotumika, jambo lililosaidia kuongeza maarifa na mbinu bora za kuimarisha huduma ya kiroho kwa waumini.