Baraka FM

Moravian Vwawa kujenga kanisa la thamani ya mil. 800

23 February 2026, 19:46

Sehemu ya jengo la kuabudia linaloendelea kujengwa katika kanisa la Moravian Jimbo la Mbozi ushirika wa Vwawa(Picha Hobokela Lwinga)

Kutumia wataalamu wenye weledi hasa katika ujenzi wa majengo kunaimarisha usalama zaidi.

Na Hobokela Lwinga

Mwenyekiti wa Jimbo la Mbozi,Kanisa la Moravian Mchungaji Lawrence Nzowa, amewataka wachungaji wa sharika zote ndani ya jimbo lake kuhakikisha wanatumia wataalamu wa ujenzi kutoka serikalini wanapojenga majengo ya kanisa,amesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga majengo yenye ubora, imara na yanayokidhi viwango vinavyotakiwa.‎‎

Mchungaji Nzowa ameyasema hayo wakati akizungumza na kituo hiki cha habari kilipotembelea Kanisa la Moravian Tanzania Ushirika wa Vwawa mkoani Songwe.‎‎

Sauti ya Mwenyekiti wa Jimbo la Mbozi,Kanisa la Moravian Mchungaji Lawrence Nzowa

Katika hatua nyingine,Mchungaji Nzowa amewapongeza waumini wa Ushirika wa Vwawa kwa jitihada wanazozifanya kumsaidia mchungaji wao,Anania Tweve, katika ujenzi wa jengo la kuabudia unaoendelea katika ushirika huo,amesema mshikamano na ushirikiano wa waumini ni chachu muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kanisa.‎‎

Mwenyekiti wa Jimbo la Mbozi,Kanisa la Moravian Mchungaji Lawrence Nzowa(Picha Hobokela Lwinga)
Sauti ya Mwenyekiti wa Jimbo la Mbozi,Kanisa la Moravian Mchungaji Lawrence Nzowa

Kwa upande wake,mchungaji wa Ushirika wa Vwawa Anania Tweve, amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo la kuabudia utakuwa wa ghorofa,na unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni mia nane hadi kukamilika kwake.‎‎

Mchungaji wa Ushirika wa Vwawa Anania Tweve(Picha Hobokela Lwinga)
Sauti ya mchungaji wa Ushirika wa Vwawa Anania Tweve

Ushirika wa Vwawa ni miongoni mwa shirika kongwe zilizoanzishwa tangu kipindi cha awali cha kuingia kwa Kanisa la Moravian katika mkoa wa Mbeya,ambao kwa sasa umezaa mkoa wa Songwe,Ushirika huo upo katika mji wa Vwawa, ambako pia ndipo yalipo makao makuu ya Wilaya ya Mbozi.‎