Baraka FM
Baraka FM
26 November 2025, 14:00

Ufundi stadi una umuhimu mkubwa katika kusaidia kunguza changamoto ya ajira kwa watu wengi.
Na Hobokela Lwinga
Wahitimu wa vyuo vya ufundi nchini wametakiwa kutumia fani zao walizosomea kwa kujiajiri ili kujiinua kiuchumi na kuachana na malalamiko ya ukosefu wa ajira.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi Mchungaji Nsevilwe Msyaliha akiwa mgeni Rasmi Katika mahafali ya tisa ya chuo cha ufundi Ilindi kinachomilikiwa na Jimbo hilo kilichopo wilaya Mbeya mkoani Mbeya.
Aidha Katibu Mkuu huyo amewataka wahitimu katika chuo hicho kuwa waaminifu katika shughuli zao hali itakayo wapa kuaminiwa na wateja wao.

Akizungumza kwa niaba Mkurugenzi wa mipango na uchumi na maendeleo kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi Esau Swillah,Afisa kilimo wa jimbo hilo Benjamin Masasi amewataka wahitimu kuzingatia ujuzi walioupata.

Hata hivyo mkuu wa chuo cha Ufundi Moravian Ilindi Paul Fataki amesema utoaji wa elimu inayotolewa chuoni hapo imekuwa ikizingatia utoaji wa elimu inayoweza kumsaidia mhitimu kujiajiri pasipo kutegemea kuajiriwa.

Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake wahitimu Agatha Anyandwile amesema chao kimekuwa msaada makubwa wa kupunguza changamoto za ajira kwa vijana wengi.
