Baraka FM

Mbunge Mbeya Vijijini achukua, kurejesha fomu kutetea kiti

1 July 2025, 19:30

Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manase Njeza akichukua fomu katika ofisi za CCM za wilaya ya Mbeya Dc

Mbunge Oran Njeza, amesema amejifunza mambo mengi katika kipindi chake cha ubunge kinachomalizika mwaka huu na kwamba yuko tayari na imara kutumia uzoefu wake huo kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wana Mbeya vijijini.

Na Josea Sinkala

Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manase Njeza, amechukua fomu ya kuomba kutetea nafasi yake ya ubunge jimbo la Mbeya vijijini ili kuendelea kusimamia shughuli za maendeleo kwa maslahi ya wananchi.

Mbunge Njeza akizungumza baada ya kuchukua fomu ya kuomba kugombea ubunge kwa mara nyingine tena, amesema ameamua kutetea nafasi hiyo ili kuendelea kuwatumikia wananchi kwani maendeleo mengi yamefanyika na yanaendelea kufanyika.

Mhe.Njeza,amechukua fomu hiyo na kuijaza kisha kuirejesha ofisini CCM Wilaya ya Mbeya ikitolewa na kupokelewa na katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini Rehema Hosea Mpagike.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Mbunge huyo wa wananchi wa Mbeya vijijini amesisitiza kuwa ni dhamira yake kuendeleza miradi ya maendeleo, kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha ustawi wa wananchi wa Mbeya Vijijini kwa ujumla wake akisema wananchi wanachohitaji ni maendeleo endelevu na si vinginevyo.

Ameongeza kuwa anaamini katika siasa za mshikamano, ushirikiano, na uwajibikaji na kwamba endapo atapewa tena nafasi ya kuendelea kuwa Mbunge basi ataendeleza usimamizi wa shughuli mbalimbali za miradi inayoendelea kwa maslahi ya wananchi.