Baraka FM

Askofu Pangani: Kwenye uchaguzi huu tuwe watu wa kusameheana

21 April 2025, 15:28

Askofu wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi mch.Robert Pangani(picha na Hobokela Lwinga)

Pasaka ni ukumbusho wa ukombozi wa mwanadamu baada ya uasi katika bustani ya Edeni.

Na Hobokela Lwinga

‎Katika kuadhimisha sikukuu ya pasaka, askofu wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi mch.Robert Pangani amewataka waumini, viongozi wa serikali na dini kuwa na moyo wa msamaha kama ambavyo Mungu alivyousamehe ulimwengu kupitia Yesu Kristo alikufa na kufufuka kwa ajili ya mwanadamu.

‎Wito huo ameutoa katika maadhimisho ya ibada ya sikukuu ya pasaka iliyofanyika katika kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi ushirika wa Ibala ulipo halmashauri ya jiji la Mbeya.

Askofu wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi mch.Robert Pangani akisalimiana na mmoja wa washirika Moravian Ibala Mbeya (picha na Hobokela Lwinga)

‎Askofu Pangani amesema ili kuwa mkristo   unayemwamini Mungu unapaswa kuwa na roho ya msamaha kwa kila mtu pasipo kujali kosa ulilofanyiwa.

‎Katika hatua nyingine amewataka watanzania kuendelea kuitunza amani ya nchi huku akiwataka wanasiasa kutokuwa na lugha za kuleta migogoro kwenye jamii kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu October,2025 ,huku akisema utunzwaji wa amani unaanzia kwenye familia.

‎Kwa upande wake mchungaji wa ushirika wa Ibala kanisa la Moravian Alinuwila Swillah amesema kila mtanzania anawajibu wa kulinda amani huku waumini walioshiriki ibada hiyo ya pasaka wakisema viongozi wa dini wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea uovu unatendeka kwenye jamii.