Baraka FM
Baraka FM
21 April 2025, 08:39

Baada ya kutokea mauaji yaliyofanywa na wananchi wenye hasira kali mkoani hapa, wachungaji wa kanisa alilokuwa anasalisha mchungaji aliyeuawa wamelaani kitendo hicho.
Na Hobokela Lwinga
Mwili wa Mchungaji Golden Ngumbuke (66) wa kanisa la Pentecoast Evangelical Fellowship of Afrika PEFA aliyefariki dunia kwa kupigwa na wananchi akiwa nyumbani kwake wakimtuhumu kumloga hadi kufa jirani yake katekista wa kanisa katoliki Fadhili Komba wa kigango cha Mwansekwa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya na mkazi wa mtaa Mwafute kata ya Ilemi jijini Mbeya umezikwa katika makaburi ya familia kitongoji cha Nyina, Kijiji Cha Lupeta, Kata Ya Swaya Wilaya Ya Mbeya Mkoani Mbeya.
Mazishi ya Mchungaji Ngumbuke yameongozwa na askofu wa kanisa la Pentecoast Evangelical Fellowship Of Afrika wilaya ya Mbeya Langson Chisunga ambaye amewataka waumini kuwa tayari wakati wote kwani kifo ni fumbo hakuna ajuaye siku wala saa ya kifo chake huku wachungaji waliofanya nao kazi walieleza nama walivyo mfahamu mchungaji Golden Ngumbuke.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupeta Edward Mwakijale ametoa neno kwa waombolezaji huku mtoto wa kwanza wa mchungaji Ngumbuke akieleza kuwa baba yao alikuwa mtumishi wa jeshi akiwa fundi wa ndege na baadaye aliacha na kuanza kazi ya kumtumkia Mungu na kwamba kifo chake kinatokana na msimamo wake katika imani na kuwa na huruma.
Mauji ya Mchungaji Ngumbuke yalifanywa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi April 17, 2025 nyumbani kwake mtaa wa Mwafute kata ya Ilemi jijini Mbeya wakimtuhumu kuhusika na kifo cha jirani katekista Fadhili Komba ambaye alifariki dunia April 15 mwaka huu baada ya kuugua kwa muda wa miezi mitano kwa madai kuwa maradhi yalimuanza baada mgogoro wa mpaka kati ya hao wawili.
