

9 April 2025, 14:12
Baada ya kipigo na kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali hatimaye marehemu amezikwa.
Na Hobokela Lwinga
Marehemu Moses Jafari Mwalemba (21), maarufu kwa jina la Vincent Jafari, ameagwa leo nyumbani kwa babu yake, Mzee Mwalemba, katika Kata ya Isanga, Mtaa wa Wigamba, Balozi wa Shina Namba 3, na anatarajiwa kuzikwa katika eneo la Isyesye, jijini Mbeya.
Marehemu alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 8, 2025, baada ya kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali katika mtaa wa Mwambenja, kata ya Iganzo, kwa tuhuma za wizi wa kuvamia na kubomoa kuta za maduka.
Diwani wa Kata ya Iganzo, Daniel Mwanjoka, amelaani vikali tukio hilo na kutoa wito kwa vijana kuachana na tabia ya wizi na badala yake wajikite katika kazi halali zitakazowasaidia kuinua maisha yao na jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwambenja, Boniface Ambilikile Syadala, kijana huyo alikamatwa na wananchi baada ya kuingia kwenye maduka matatu kwa njia ya dari, akishirikiana na wenzake waliokuwa nje. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na limeonya vikali tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.