

8 April 2025, 20:09
Vijana wengi wamekua wakipoteza maisha kutokana na kujihusianisha na vitendo vya kihalifu ambavyo wamekuwa wakifanya kwa kizingizio cha ukosefu wa ajira.
Na Hobokela Lwinga
Mkazi mmoja wa Iganzo, Vincent Jafari (21), amefariki dunia baada ya kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali usiku wa kuamkia Aprili 8, 2025, katika mtaa wa Mwambenja, kata ya Iganzo, jijini Mbeya.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Iganzo, Daniel Mwanjoka, amelaani vikali tukio hilo na kuwataka vijana kujiepusha na vitendo vya wizi na badala yake wajishughulishe na kazi halali kwa ajili ya kujenga maisha yao na jamii kwa ujumla.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mwambenja, Boniface Ambilikile Syadala, amesema kuwa kijana huyo alikamatwa na wakazi wa eneo hilo baada ya kuingia kwenye maduka matatu kwa njia ya dari, akisaidiana na wenzake waliokuwa wakisubiri nje kwa ajili ya kutekeleza wizi huo.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini washiriki wengine wa tukio hilo, huku likitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola.