

20 March 2025, 17:39
Kutokana na kaulimbiu ya chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) isemayo “No Reform No Election” Kanda ya Nyasa wametangaza kuanza mikutano ya hadhara kuelimisha maana ya kaulimbiu hiyo.
Na Hobokela Lwinga
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa kimetangaza kuanza kwa mikutano ya hadhara katika mikoa ya kanda hiyo kuanzia Machi 23, 2025, kwa lengo la kuwaeleza wananchi msimamo wa chama huo wa “No Reform, No Election”.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya Machi 20, 2025, katika ofisi za kanda hiyo, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Osmund Mbilinyi Sugu, amesema mikutano hiyo itazinduliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Tundu Antipas Lissu, ambaye ataongoza mikutano ya hadhara na vikao vya ndani katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa.
Aidha, Makamu Mwenyekiti Bara, John Wegesa Heche, ataanza mikutano hiyo mkoani Mbeya, kisha kuendelea na Njombe na hatimaye kufunga mikutano hiyo mkoani Iringa kabla ya kuelekea kanda nyingine.Katika mikutano hiyo, ajenda kuu itakuwa kuwaeleza wananchi umuhimu wa mabadiliko ya mifumo na sheria za uchaguzi ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika kwa haki, uhuru, na amani.
CHADEMA imesisitiza kuwa iwapo hakutakuwa na marekebisho ya sheria hizo, chama hicho kitasimamia msimamo wake wa kushinikiza wananchi kususia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Tanzania Bara, Elizabeth Mwakimomo, amesema chama hicho kitaendelea kuwa tumaini la wananchi kwa kutetea maslahi ya taifa, ikiwemo kupigania katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, na mabadiliko ya sheria za uchaguzi.
Mwakimomo ameongeza kuwa wanawake ndani ya CHADEMA ni jeshi linalosimama imara katika kupigania mabadiliko ya kweli yanayolenga kuhakikisha viongozi wanaopatikana ni wale wenye moyo wa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.Ziara ya viongozi wa CHADEMA Taifa katika Kanda ya Nyasa itadumu kuanzia Machi 23 hadi Machi 29, 2025, ambapo chama hicho kitakutana na wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara na vikao vya ndani.
Pia, ziara hiyo itaambatana na kampeni ya “No Reform, No Election” inayosisitiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi, pamoja na kampeni ya “Tone Tone”, inayohimiza wanachama na wananchi kuchangia chama ili kiweze kujiendesha. Baada ya Kanda ya Nyasa, CHADEMA kitaendelea na mikutano ya aina hiyo katika kanda nyingine nchini kuelekea uchaguzi mkuu.