Baraka FM

Dereva bajaji ajinyonga Mbeya kisa kushindwa kupeleka fedha kwa boss

6 March 2025, 09:47

Picha na mtandao

Hali hii sasa imekuwa kawaida kwa madereva wa bajaji kuchukua hatua za kujiua kisa kushindwa kurejesha malengo kwa maboss zao,mamlaka ziingilie kati kuhusu mikataba ya ya madereva wengi

Na Ezekiel Kamanga

Siku chache baada ya dereva wa Bajaj mkazi wa Iganzo kufariki kwa kujinyonga dereva mwingine wa Bajaj Isaya Edwin(26) amefariki kwa kujinyonga chumbani kwake machi 4,2025 majira ya saa sita mchana wakati mkewe akifua nguo nje ya nyumba waliyopanga.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyibuko Kata ya Iyela Jijini Mbeya Titus Virumba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo linalodaiwa kutokea machi 4,2025 majira ya saa sita mchana.

Virumba amesema alipata taarifa kutoka kwa mwenye nyumba na mke wa marehemu ambapo alitoa taarifa kwa Polisi Kata na baadae maafisa wengine wa Polisi walifika na kukata kamba kisha kuushusha mwili na baadaye kwenda hospitali kwa uchunguzi zaidi.

Picha ya marehemu Isaya Edwin

Hata hivyo Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyibuko amesema marehemu hajaacha ujumbe wowote na ameacha watoto watatu, Virumba amesema sababu kubwa za vifo kwa vijana wengi vinatokana na majukumu makubwa ya kifamilia huku wakiwa na umri mdogo Sababu nyingine imetajwa kukithiri kwa michezo ya bonanza, pool na kamali mitaani vijana wengi huingia tamaa ya kucheza na wanapokosa ndipo huchukua hatua za kujitoa uhai hivyo ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuiondoa michezo hiyo Ili kuwanusuru vijana.

Neema Jonson ni mke wa Marehemu amesema mumewe kabla ya kujinyonga amepitia mikasa mbalimbali ikiwemo kunyang’anywa Bajaj mbili za mkataba pia kunyang’anywa Bajaj nyingine aliyokuwa akiiendesha baada ya kushindwa kufikisha malengo hivyo sababu kubwa ya kifo cha mumewe ni msongo wa mawazo.

Mmiliki wa Bajaj Rhoda Mwano amekanusha kumnyang’anya marehemu Bajaj amesema hadi kifo kinamkuta Bajaj ilikuwa mikononi mwake na alipofuatilia alibaini kuwa Bajaj yake inaendeshwa na mtu mwingine(deiwaka)na baada ya kupata taarifa za kifo ndipo akaiegesha eneo jingine.

Aidha amesema waliingia mkataba na marehemu mwezi Juni mwaka jana na mkataba ulikuwa umalizike mwezi Aprili mwakani.