Baraka FM

Serikali yaleta neema maji Mbuyuni,kero ya maji sasa basi

20 February 2025, 07:49

Utiaji wa saini ya utatuzi wa changamoto ya maji Ruaha Mbuyuni (picha na Moses Mbwambo)

Maji ni uhai palipo na maji ndio sehemu viumbe hai vinaweza kustahimili kuishi,maji yanatumiwa na binadamu,mnyama,ndege hata wadudu.

Na Moses Mbwambo, Iringa

Serikali ya Awamu ya Sita kupitia wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA imetoa zaidi ya shilingi Millioni 271 kwaajili ya uboreshaji wa mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo,mradi ambao unaenda kuondoa adha ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Akizungumza leo Februari 19, 2025 wakati akishuhudia zoezi la utiaji saini, uboreshaji wa mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni Wilayani Kilolo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Serukamba ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo zinazoenda kumaliza changamoto ya maji safi ma salama katika eneo hili.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Serukamba (picha na Moses Mbwambo)

Mhe.Serukamba ameongeza kwa kuwasisitiza wakandarasi walio saini mkataba huo kufanya kazi kwa Haraka na kwa ubora ili kuwezesha Wananchi wa kijiji cha Ruaha Mbuyuni na Msosa kupata huduma ya maji safi na salama .

Aidha Mhe. Serukamba amewaagiza RUWASA na Tume ya Umwagiliaji Mkoa wa Iringa kuwasimamia ipasavyo wakandarasi wa miradi hiyo kwa kuhakikisha miradi inakamilika kwa Wakati.

Uboreshaji huo wa mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni utahudumia Vijiji Viwili vya Msosa na Ruaha Mbuyuni vyenye jumla ya watu wapatao 34,028.