Baraka FM

Mbeya wafikiwa na msaada wa kisheria wa Mama Samia legal aid,wanaume waitwa kutoa kero za ndoa

19 February 2025, 21:30

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera

Wakati kampeni ya uzinduzi wa msaada wa kisheria wa mama Samia legal aid ukiwa umefanyika katika mikoa kumi na saba, sasa wananchi mkoa wa Mbeya wamefikiwa.

Na Hobokela Lwinga

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Comrade Juma Zuberi Homera amewataka wananchi mkoani Mbeya kujitokeza kwa wingi katika kampeni ya msaada wa kisheria inayojulikana kama mama samia legal aids campaign.

Homera ametoa wito huo wakati akizungumza wanahabari ofisini kwake,amesema huduma hiyo itaanza February 24 hadi machi 05,2025 katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema huduma hiyo inalenga kupunguza malalamiko ya wananchi katika sekta ya sheria pamoja na kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani na katika vyombo vingine vya kutoa haki.

Aidha Homera amewataka wananchi waendelee kufuatilia vyombo vya Habari kwa ajili ya kupata ratiba na utaratibu wa kupata huduma hiyo kupitia halmashauri zao.

Sambamba na hayo amesema watu wa makundi yote wanapaswa kujitokeza kutoa kero zao wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na wanaume kujitokeza kutoa kero wanazokutana kwenye maisha yao ndoa.

Hata hivyo mratibu wa kampeni hiyo,wakili wa serikali kutoka wizara ya katiba na sheria Emmanuel Mbega amesema kampeni hiyo itakuwa ya siku kumi kwa mkoa wa Mbeya ambapo italenga kutatua migogoro ya ardhi,ndoa,mirathi,wakulima na wafugaji,ukatili wa kijinsia usajili wa vizazi na vifo kupitia wakala wa usajili na ufilisi (RITA)sambamba na utoaji wa elimu ya maswala ya kisheria.

Utoaji wa huduma ya mama Samia legal AIDS unakwenda na kauli mbiu isemayo “Msaada wa kisheria kwa haki na usawa, amani na maendeleo”.