Baraka FM

DC Itunda aipongeza mahakama ya wilaya Songwe kwa utendaji kazi mzuri

4 February 2025, 13:04

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda

Ufanyaji kazi mzuri huwa unamweka mtu sehemu nzuri ya kusemwa na watu na hali hiyo huwa inafanya kupongezwa iwe kwa taasisi au mtu binafsi.

Na Ezekiel Kamanga

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda ameipongeza Mahakama ya Wilaya ya Songwe kwa kufanya kazi nzuri ya kutoa haki kwa wananchi hali iliyosababisha kutokuwa na malalamiko katika Wilaya hiyo.

Pia, Mhe. Itunda ameishukuru Mahakama kwa kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zinziojitokeza katika Wilaya ya Songwe.

Mkuu wa Wilaya huyo ametoa pongezi hizo leo Jumatatu Februari 3, 2025 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiku ya Sheria ambayo kiwilaya yamefanyika katika Viwanja vya mahakama ya Wilaya ya Songwe.

Aidha, DC Itunda amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mahusiano hususani katika kutekeleza falsafa ya 4R pamoja na kuunda Tume ya Haki Jinai.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Songwe, Augustino Lugome amesema katika wiki ya sheria wametoa elimu kwa wananchi na makundi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Songwe.

Amesema kuwa maeneo ambayo walipata ushirikiano mkubwa na kutoa elimu ni pamoja na maeneo ambayo yanafanywa shughuli za uchimbaji madini.

Pia, amesema kuwa katika kipindi hicho cha wiki moja wamesaidia wananchi wengi katika kutoa elimu hasa katika masuala yanayohusiana na changamoto za ardhi.