

4 February 2025, 13:24
Biblia inasema “Kutoka 24:4-5
[4]Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli,
[5]akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng’ombe.”
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Lumbila Kata ya Iwambi Jijini Mbeya limeanza harambee ya kukusanya pesa za ujenzi wa Kanisa la kisasa litakaloghalimu zaidi ya shilingi milioni mia awamu ya kwanza wanatarajia kukusanya shilingi milioni hamsini ifikapo mwezi septemba 2025 mpaka sasa Kanisa limekusanya jumla ya shilingi milioni kumi na nane.
Akitoa taarifa katika ibada Mchungaji Fadhili Yona Sanga wa Ushirika wa Lumbila amesema yeye atachangia shilingi laki tano katika ujenzi huo huku akiwaomba Waumini kulipa kipaumbele suala hilo.
Aidha amesema ni wakati mzuri wa kila mmoja kushiriki kujenga hekalu la Bwana.
Mchungaji Sanga amewataka Waumini kuamini katika maombi kwani maombi yana majibu sahihi huku akibainisha kuwa Kanisa lipo katika mfungo wa maombi ya siku arobaini.
Hata hivyo Mchungaji aliongoza ibada maalumu ya maombi kwa ajili ya kupanda sadaka ya mbegu kwa mwaka 2025.
Wakati hayo yakijiri Mchungaji Isaya Mwamlima wa Kanisa la Moravian Tanzania Ushirika wa Msia Jimbo la Mbozi amewataka Waumini kufanya maombi kwa ajili ya Kanisa na Taifa Ili tuvushwe salama.
Mwamlima ameongoza ibada ya maombi katika Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Lumbila kuombea mambo mbalimbali katika familia,Kanisa na Taifa kwa ujumla.