

29 January 2025, 16:34
Jukumu la kupambana na kuzuia Rushwa si la taasisi ya TAKUKURU pekee bali kila mwananchi anao wajibu wa kutoa taarifa za Rushwa pindi anapobaini mianya katika eneo alilopo.
Na Hobokela Lwinga, Mbeya
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Mbeya imefanikiwa kurejesha fedha zaidi ya milioni 15 kwa wananchi kutoka taasisi ya kimarekani inayoitwa Henry Jackson foundation medical research international HJFRMI yenye makao makuu yake mkoani Mbeya.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya miezi mitatu kuanzia October hadi disemba 2024,Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya Maghela Ndimbo amesema taasisi yake imeshinda kesi hiyo dhidi ya bw.Emmanuel Malewo ambaye alijipatia kama rushwa kwa wasafirisha sampuli za binadamu katika wilaya ya Mbarali.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya amesema wamebaini uwepo wa mianya ya upotevu wa mapato yatokanayo na ukataji wa leseni za biashara katika halmashauri ya jiji la Mbeya.
Aidha amesema TAKUKURU mkoa wa Mbeya umefanikiwa kuwafikia wananchi 54,224 kwa kuwapatia elimu ya kuzuia vitendo vya Rushwa.
Sanjari na hayo Ndimbo amesema kwa miezi mitatu ijayo January hadi machi itaendelea na ya TAKUKURU Rafiki kwa kufanya mikutano ya hadhara kila mwezi kwa ngazi ya kata kwa lengo la kuibua kero mbalimbali.
Mkuu huyo wa TAKUKURU ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kufuatilia na kuhoji hatua za utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao ili kudhibiti ubadhirifu wa fedha za miradi hiyo.