

28 January 2025, 18:19
Changamoto ya miundombinu ya barabara katika maeneo mengi ya jiji la Mbeya yamekuwa kero kwa madereva na wananchi.
Na Josea Sinkala, Mbeya.
Madereva wa pikipiki za magurudumu matatu almaarufu Bajaji wanaofanya safari zao kati ya Isyesye na Kabwe Mwanjelwa jijini Mbeya, wamelazimika kufunga barabara kwa saa kadhaa ili kuishinikiza Serikali kuwahimiza wakandarasi wanaojenga barabara ya Isyesye mwisho wa lami hadi Gombe kaskazini Itezi kujenga kwa wakati na kuondoa vikwazo kwenye barabara hiyo kutokana na barabara za muda kutokuwa rafiki.
Madereva Bajaji wakizungumza katika eneo la Isyesye sokoni, wamesema wanao uwezo wa kusubiri barabara kubwa imalizike kujengwa lakini kero kubwa ni kuona barabara za muda walizoelekezwa kupita kwa sasa zikiwa sio rafiki kwa vyombo vyao na abiria pia hususani wagonjwa na wajawazito kutokana na ubovu uliokithiri huku barabara inayojengwa ikiwa imezuiwa kwa magari makubwa ya kutengenezea barabara.
Kadhia hiyo ya madereva inashuhudiwa pia kwa abiria ambao licha ya kusafiri kwa tabu lakini wamekuwa wakipandishiwa kiwango cha nauli kutoka shilingi mia nane na kutozwa shilingi elfu moja hadi elfu mbili kwa abiria mmoja jambo ambalo limekuwa kadhia kubwa na kuwakwamisha kiuchumi.
Diwani wa kata ya Isyesye Mhe. Ibrahim John Mwampwani amesema tayari wakandarasi wameondoa magari ya ujenzi katikati mwa barabara na vifusi vimeanza kuchimbwa ili kupelekwa kwenye barabara inayotumika kwa muda na madereva hao ili kuikarabati ipitike kwa urahisi wakati ujenzi unaendelea kwenye barabara ya Isyesye Gombe.