Baraka FM

MWEF yatoa msaada hospitali ya wazazi Meta

27 December 2024, 09:21

Baadhi ya wanakikundi cha MWEF wakiwa katika Hospitali ya wazazi Meta(picha na Ezekiel Kamanga)

Taasisi ya Maryprisca Women Impowerment Foundation(MWEF)inayoongozwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi imetembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa ajili ya kutoa msaada kwa wazazi waliojifungua siku ya sikukuu ya Christmas.

Na Ezekiel Kamanga

Mwenyekiti wa Taasisi ya Maryprisca Women Impowerment Foundation Adam Simbaya amesema lengo la kutembea Hospitali ya wazazi Meta(Mbeya) ni kumshukuru Mungu pia akianisha zawadi zilizotolewa kuwa ni pamoja na maziwa, sabuni,pampas na wipes.

Mmoja wawanufaika katika mgao huo akikabidhiwa zawadi(picha na Ezekiel Kamanga)

Aidha Simbaya amesema wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye amekuwa akiyagusa makundi mbalimbali yakiwemo ya wanawake na watoto.

Scolastica Kapinga ni muuguzi wa zamu kwa niaba ya uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Kitengo cha Wazazi Meta ameishukuru Taasisi hiyo kwa kutoa msaada kwa wazazi na watoto sanjari na maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali yamefanya watoe huduma kwa ufanisi mkubwa.

Kapinga amesema jumla ya watoto 18 wamezaliwa siku ya sikukuu ya Christmas tisa wakiwa ni wa kiume na tisa wa kike.

Wanachama wa MWEF wakiwa toka katika Hospitali ya wazazi Meta(picha na Ezekiel Kamanga)

Afisa Ustawi wa Jamii Wiberd Mussa ameishukuru Taasisi kwa upendo kuwakumbuka watoto huku akiwataka wadau wengine kujitokeza kutoa misaada kwa wazazi na watoto ambao baadhi hutoka nje ya Mkoa wa Mbeya.

Tusekile Abel na Hafsa Hassan ni wazazi waliojifungua watoto mapacha kila mmoja wameishukuru Taasisi kwa kuwapa msaada pia wakiwashukuru madaktari na wauguzi kwa huduma nzuri.