Waumini watakiwa kujifanyia tathimini katika kusherekea Christmas ikiwa ni pamoja na kuacha dhambi
25 December 2024, 12:44
Wakristo duniani kote wanasherekea sikukuu ya kuzaliwa Yesu Kristo ambapo katika mahubiri mbalimbali yamewakumbusha waumini kumrejea Mungu.
Na Yuda Joseph Mwakalinga
Waumini wa madhehebu mbalimbali nchini,wametakiwa kutumia maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kama fursa ya kujitathmini kiroho na kuachilia magumu yote waliyopitia.
Wito huo umetolewa leo katika ibada ya Krismasi iliyofanyika kanisa la Moravian jimbo la kusini magharibi ushirika wa igurusi , ikiongozwa na Mchungaji Braison Mwampashi.
Mchungaji Mwampashi, akihubiri kutoka katika kitabu cha Martha 2:7, alisisitiza kwamba Krismasi ni siku muhimu katika historia ya imani ya Kikristo kwani inakumbusha kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu Kristo.
Ameleza kuwa mafanikio na changamoto zote zinazoendelea katika maisha ya waumini ni matokeo ya neema na upendo wa Yesu Kristo.
“Tumefika mwezi wa Desemba kwa neema ya Mungu. Ni ishara ya wema wake kwetu licha ya magumu mengi ambayo tumepitia. Ni wakati mwafaka kwa kila mmoja kujitathmini na kumkaribisha Yesu azaliwe ndani ya mioyo yetu,” amehubiri Mchungaji Mwampashi.
Ibada hiyo imekuwa na uzito wa kiroho, ikiwakumbusha waumini kwamba Krismasi siyo tu sherehe, bali ni wakati wa kuimarisha uhusiano wao na Mungu, kutafakari baraka zake, na kujikita zaidi katika kuishi maisha ya imani, upendo, na kumtumikia Mungu kwa dhati.