Baraka FM

Mhandisi Mahundi anadi wagombea CCM Mbeya

26 November 2024, 08:19

Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa Mhandisi Marryprisca Mahundi (wa pili kulia)

Tanzania inakwenda kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na viongozi Novemba 27, 2024 ambao unatoa fursa ya wananchi kuwachagua viongozi wanaowataka.

Na Ezekiel Kamanga

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa ameendelea na kampeni ya kuwanadi wagombea mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya.

Akiwa Kata ya Bwawani Mamlaka ya Mji mdogo wa Makongolosi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka wananchi kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi kwani ndicho Chama pekee kitachowaletea maendeleo.

Mahundi ameitaja baadhi ya miradi inayotekelezwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni pamoja na ujenzi wa shule za msingi na Sekondari, miradi ya maji, Vituo vya afya na miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca kwa kipindi cha siku mbili ameweza kufanya kampeni ya kuwanadi wagombea katika Halmashauri za Mbeya, Rungwe na Chunya.