Baraka FM

Wananchi watakiwa kuwa na uzalendo kipindi hiki cha uchaguzi

9 November 2024, 07:15

Viongozi wa dini Songwe Watoa Miongozo kwa Wananchi Kuhusiana na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Na Mwandishi wetu,Songwe

Katika Mkoa wa Songwe, wananchi wametakiwa kuweka uzalendo mbele katika kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha wanachagua viongozi bora na siyo viongozi bora pekee.

Wito huu umetolewa na viongozi wa amani wa Mkoa wa Songwe katika kikao cha pamoja na Waandishi wa habari kilichofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Songwe Hussein Batuza, amesema kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unapaswa kuongozwa na uzalendo na amani, huku wananchi wakiwepo katika mchakato wa kuchagua viongozi ambao watatekeleza majukumu yao kwa ustawi wa jamii bila kubagua dini, kabila au itikadi yoyote.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa dini kutoa elimu kwa waumini wao ili wajiandae na kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura.

Naye Katibu wa Kamati ya Amani Mkoa wa Songwe Rojas Simkonda, amewasihi wananchi kuepuka kushawishika kwa rushwa ya aina yoyote inayotolewa na wagombea ili kupata kura zao. Amefafanua kuwa ununuzi wa vitu au ahadi za kifedha ni rushwa na kwamba uchaguzi lazima uwe huru na wa haki, ambapo kila mtu atachaguliwa kwa uwezo wake na siyo kwa matumizi ya fedha.

Abdala Msolomi Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Songwe ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia ustawi wa wazee wakati wa kupiga kura, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wazee wanasaidiwa ili waweze kushiriki kwenye zoezi hilo bila shida yoyote, hasa kutokana na changamoto za kiafya na nguvu.

Kwa upande mwingine Kiongozi wa Kimila, Chifu Sibhelwa Nzunda, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuhudhuria kampeni za wagombea ili waweze kutathmini na kuchagua kiongozi wanayemwamini, anayekidhi matarajio yao. Ameongeza kuwa uchaguzi ni haki ya kila raia, na hivyo ni muhimu kushiriki kwa ari na bila ushawishi wowote.

Kikao cha amani kilichofanyika mkoani Songwe kimejumuisha wawakilishi viongozi wa dini zote pamoja na wazee wa mila, ambapo walijadili kwa kina masuala ya amani na umuhimu wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia sheria.