Baraka FM

176 wakamatwa kwa tuhuma mbalimbali Mbeya, yupo aliyeua mke kisa wivu wa mapenzi

5 November 2024, 20:07

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga

Polisi wamekuwa na wajibu kulinda usalama na kulinda raia na Mali zao hivyo wananchi hawana budii kutoa ushirikiano pindi wanapoona uhalifu na uvunjifu wa amani.

Na Hobokela Lwinga, Mbeya

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 176 wakiwemo wa matukio ya mauaji, dawa za kulevya, uvunjaji na wizi, nyara za serikali na pombe haramu ya moshi.

Akizungumza na vyombo vya habari kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema wanawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara ya madini Peter Bruno Mteta [59] mkazi wa matundasi Wilayani Chunya tukio lililotokea Oktoba 12, 2024 saa 2:00 usiku kwa kumpiga risasi mgongoni akiwa nyumbani kwake.

Aidha katika tukio lingine Jeshi la Polisi linamshikilia Hamis Shizya Kasunga [50] mkazi wa maghorofani Jijini Mbeya kwa tuhuma za kumuua mke wake aitwaye Emmy Fred Mwasile [35] mkazi wa Forest Maghorofani Jijini Mbeya kwa kumpiga kwa kitu kizito sehemu mbalimbali za mwili wake.

Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia na katika ufuatiliaji alikamatwa Novemba 23, 2024 saa 9:00 alasiri katika mji mdogo wa Tunduma Mkoani Songwe akiwa katika harakati za kuvuka mpaka kwenda nchini Zambia.

Vile vile jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 23 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uvunjaji wa nyumba na kuiba katika maeneo tofauti ya Mkoa wa Mbeya.

Hata hivyo katika muendelezo wa misako iliyofanywa na Jeshi la Polisi mkoani hapa watuhumiwa wengine 31 wamekamatwa kwa nyakati tofauti kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa kilo 18 na gramu 820, pombe haramu ya moshi maarufu gongo ujazo wa lita 104 na mtambo mmoja wa kutengenezea pombe hiyo.