Baraka FM

Mahafali ya chekechea Anu daycare yafana jijini Mbeya

5 November 2024, 16:35

Na Yuda Joseph Mwakalinga

Mahafali ya wanafunzi wa shule ya chekechea ya Anu Daycare and Kindergarten iliyopo Sabasaba jijini Mbeya yalifanyika kwa mafanikio makubwa, huku wazazi na walimu wakishirikiana katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa watoto wao.

Katika hotuba yake Mdau wa maendeleo ya elimu Margareth Muindi amewataka wazazi kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya watoto wao na kupunguza kujishughulisha sana na kazi akisisitiza umuhimu wa kuwalea watoto katika mazingira bora ya malezi na elimu.

Mdau wa maendeleo ya elimu Margareth Muindi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shule hiyo Anuciata Ngonyani amesisitiza umuhimu wa watoto kuhudhuria shule badala ya kubaki nyumbani ili kupunguza ajali na hatari zinazowakabili watoto wadogo.

Ameonya pia dhidi ya tabia ya kuwahamisha watoto kutoka shule moja kwenda nyingine bila sababu za msingi, akisema kuwa kufanya hivyo ni “laana” kwa watoto na kunawaathiri kisaikolojia.

Mkurugenzi wa shule hiyo Anuciata Ngonyani

Wazazi waliohudhuria mahafali hayo walitoa shukrani zao kwa walimu kwa kujitolea kwao na huduma bora walizozitoa kwa watoto wao, wakisema wameona mabadiliko makubwa katika maendeleo ya watoto wao.

Wanafunzi nao walipata fursa ya kutoa shukrani zao kwa huduma nzuri walizopokea na kuelezea utayari wao kuanza elimu ya msingi.