Mikutano ya idara ya uinjilisti Moravian yatajwa sababu kukua kwa kanisa
5 November 2024, 15:43
Kanisa la Moravian Tanzania limekuwa na utaratibu wa kuandaa Mikutano mbalimbali ya idara inayofanyika katika majimbo lengo likiwa ni kueneza injili ya kristo.
Na Deus Mellah
Uwepo wa idara za Uinjilisti katika Kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kusini Magharibi unatajwa kusaidia kukua kwa kanisa kutokana na kazi zake kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Mch. Asulumenye Mwahalende wakati akizungumza katika mkutano wa idara ya uinjilist jimbo uliofanyika ushirika wa Chimala.
Mch. Mwahalende ameziomba shirika zote ambazo hazina idara ya uinjilisti kuwa nazo kwani ni msaada mkubwa kwa kanisa.
Naye Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian wilaya ya Mbarali Amos Mwampamba amesema mkutano huo umeleta mafanikio makubwa kwa wakazi wa kata ya chimala.
Aidha katibu wa idara ya uinjilist jimbo Mch. Peter Mbughi amesema mafanikio ya idara hiyo ni makubwa kwa kuwa watu wengi wameendelea kuokoka baada ya kufikiwa na huduma hiyo.
Nao baadhi ya waimbaji walioshiriki katika mkutano huo wamesema mikutano hiyo imekuwa ikiwajenga kiroho na kimwili