Moravian Chunya yawapa kicheko watu wenye mahitaji maalum
4 November 2024, 19:45
Kila binadamu mwenye pumzi ya uhai unapaswa kupata mahitaji mbalimbali muhimu pasipo kujali hali yake ya maumbile,au maisha kwa ujumla.
Na Hobokela Lwinga
Serikali na taasisi binafsi zimetakiwa kuwa mstari wa mbele kusaidia makundi maalumu yenye uhitaji ikiwemo yatima,wajane na watu wenye shida mbalimbali kwani kufanya hivyo kutapunguza changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili.
Wito huo umetolewa na mchungaji wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi ushirika wa Chunya Godfrey Tinga katika Ibada ya ugawaji wa misaada mbalimbali kwa watu wenye mahitaji maalum ndani ya halmashauri ya Chunya.
Aidha mchungaji Tinga amesema kuhudumia wahitaji ni agizo la Mungu kwenye vitabu vitakatifu hivyo kanisa Lina wajibu wa kutunza na kulea makundi hayo.
Kwa upande wake kiongozi wa udiakonia chunya mjini Rabson Kalua amesema misaada yote iliyotolewa kwa wahitaji hao imetokana na michango ya waumini Moravian Chunya huku akisema tangu wameanza kuhudumia makundi hayo wamefanikiwa kuzipatia bima ya afya baadhi ya kaya.
Nao baadhi ya waratibu na viongozi wa Udiakonia katika ushirika wa Chunya wamesema mafanikio ya tukio hilo yametokana na ushirikiano walioupata kutoka kwa kanisa.
Baadhi ya wanufaika wa msaada huo wakiwemo watoto na wazazi wameshukuru kwa kuwezeshwa huku wakisema utawasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili.
Ushirika wa Chunya Moravian wamekuwa na utaratibu kila mwaka kuwa na ibada ya kuwapatia mahitaji watu wenye mahitaji maalum kwa kuwasaidia yatima kuwapatia vifaaa vya shule, mavazi na na watu wazima kuwapatia nguo na kushiriki chakula kwa pamoja.