Wasioona waoana na wamejaliwa kupata mtoto anayeona Mbeya
4 November 2024, 19:22
Unawaza ukadhani ni simulizi lakini hii habari ya kwel kwa wanandoa wenye ulemavu wa kutoona kuamua kuishi pamoja.
Na Ezekiel Kamanga
Upendo Tebela(37)na mumewe Mwakifumbwa(52) wakazi wa Mbalizi wote ni vipofu waliamua kuoana mwaka 2021 na wamejaliwa kupata mtoto wa kiume aitwaye Agape mwenye umri wa miezi kumi na moja wametoa somo kwa jamii baada kukataa kutembea mitaani kuomba omba badala yake wamekita kwenye sanaa ya ususi wa vitambaa, vikapu na stool.
Upendo Tebela amesema alipatwa na upofu akiwa na umri wa miaka saba na wazazi wake walijitahidi kumtafutia matibabu bila mafanikio.
Naye Mwakifumbwa amesema alipatwa na upofu wa macho akiwa na umri wa miaka mitano wazazi wake walijitahidi kumpatia tiba lakini ilishindikana.
Wote wameikubali hali hiyo ambapo walikutana kwenye vikao vya wasioona ndipo walipopendana na kuamua kuoana ndoa ya Kikristo katika Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Mbalizi II mwaka 2022 na walijaliwa kupata mtoto wa kiume miezi kumi na moja iliyopita.
Upendo amejikita kufuma vitambaa vya mezani,masweta,pochi na sox ambapo huuza Ili kujikimu na maisha ambapo pochi huziuza shilingi elfu hamsini.
Aidha Mwakifumbwa amesema changamoto za maisha ndizo zimemfanya ajifunze kutengeneza stool za kamba za manila ambapo stool moja huiuza shilingi elfu kumi na tano.
Wanandoa hao wamebainisha changamoto katika kazi zao ni upatikanaji wa wateja kutokana na kazi zao kuzifanyia nyumbani na zaidi hutegemea kuuza bidhaa zao siku ya Jumapili kwenye makanisa mbalimbali.
Kwa pamoja wameomba wadau kuwaongezea mtaji na kuwatafutia masoko pia hawajabahatika kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri.
Changamoto nyingine ni pamoja na kukosa bima ya afya pindi wanapoumwa hivyo wanaiomba jamii itakayoguswa kuweza kuwasaidia bima za Afya kwa yeye, mtoto na mumewe.
Pia wanakabiliwa na pesa za kulipa pango la nyumba ambapo hulipa shilingi elfu thelathini kila mwezi hivyo wakikosa wateja wa kununua bidhaa zao maisha huwa magumu kwao.
Upendo Tebela pamoja na upofu alionao lakini anawajibika kufanya kazi kama mwanamke kama kufua,kupika na kuosha vyombo.
Tebela anasema akipika mara zote hutamani kula na mumewe na chakula anachopendelea mumewe ni pamoja na ugali samaki na mboga za majani.
Wanandoa hao wanapinga tabia ya watu wasioona kupita mitaani kuomba omba badala yake wajifunze shughuli itakayowapatia kipato.
Matamanio yao ni kuwa na watoto watatu pia wakipata mfadhili wanunue nyumba Ili kuondokana na kadhia ya kudaiwa pango kila mwezi.
Wadau watakaoguswa wanaweza kutoa sadaka yao kupitia namba 0753759886