CCM Mbeya yaridhishwa na zoezi la uandikishaji daftari la mpiga kura
17 October 2024, 19:54
November 27,2024 Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ambapo kwa sasa zoezi la uandikishaji linaendelea.
Na Hobokela Lwinga
Wakati leo ikiwa ni siku ya saba tangu zoezi la wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Mbeya kimesema kuwa kimeridhishwa na namna wananchi wa mkoa huo walivyoitikia wito wa kujiandakisha akisisitiza wananchi wengine kujitokeza kwani ni haki yao.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Katibu mwenezi wa chama hicho mkoa wa Mbeya Christopher Uhagile amesema kuwa hadi kufikia leo hali ya wananchi kwenda kujiandikisha inakwenda vizuri.
Uhagile ameongeza kuwa suala la kujiandikisha ni haki ya kila mtu akisema zoezi linaloendelea sasa ni wananchi kujiandikisha katika daftari la mpiga kura na si daftari la kudumu la mpiga kura akisihi wananchi kutochanganya jambo hilo.
Kuhusu malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa kutokana na zoezi hilo la kujiandikisha linaloendelea katibu huyo mwenezi wa CCM mkoa Wa Mbeya amewataka wanaolalamika kupeleka hoja zao kwenye Tume Ya huru ya Uchaguzi ili ziweze kufanyiwa kazi.