Tulia Trust yatoa mifuko 50 ya saruji shule ya msingi Ikule Rungwe
12 October 2024, 18:25
Ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi jamii haina budii kuweka mazingira mazuri kwa kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki kwa wanafunzi.
Na Ezekiel Kamanga
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson kupitia Taasisi yake ya Tulia Trust imetoa msaada wa mifuko hamsini ya saruji kwa shule ya Msingi Ikule Kata ya Masebe Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya kwa ajili ya kukarabati ofisi ya walimu ambapo kwa sasa wanatumia moja ya darasa kama ofisi.
Msaada huo umekabidhiwa na Afisa Habari wa Taasisi ya Tulia Trust Joshua Mwakanolo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tulia Trust Dkt Tulia Ackson.
Mwakanolo amesema Taasisi ilipokea maombi kutoka uongozi wa shule hiyo hivyo kwa kutambua umuhimu wa elimu Taasisi imewiwa kutoa msaada huo Ili kuchochea ubora wa elimu sanjari na kuungana na Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Innocent Atilyo ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amesema sehemu kubwa ya shule hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi ikiwa na madarasa saba na jumla ya watoto zaidi ya mia mbili thelathini ambapo Serikali imetoa milioni thelathini na tano nukta tisa kwa mwaka 2021/2022 kuungana na wananchi.
Bedon Mwasubila ni Diwani wa Kata ya Masebe mbali ya kumshukuru Dkt Tulia Ackson kwa kutoa msaada huo pia amewashukuru wadau mbalimbali wanaochangia ujenzi wa shule hiyo.
Japheth Jema Mwenyekiti wa CCM Kata ya Masebe ameipongeza na kuishukuru Taasisi ya Tulia Trust kupitia Mkurugenzi wake Dkt Tulia Ackson.
Afisa elimu Kata ya Masebe Otino Mwampamba ameishukuru Taasisi ya Tulia Trust kwa kutoa msaada wa mifuko hamsini ya saruji kwani itachochea ufanisi kwa walimu ambao hawana ofisi kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Masebe Emmanuel Mwakyambiki amesema msaada umekuja kwa wakati kwani utawapunguzia michango.
Shule hiyo yenye walimu watano ,wanne wa kiume na wa kike mmoja imeanzishwa miaka ya 1960 imekuwa ikikua kitaaluma siku hadi siku.