Mch.Mwahalende azindua ofisi za wilaya ya Mbalizi kanisa la Moravian
8 October 2024, 00:29
Ni utaratibu wa kikatiba kila ngazi ya kanisa la moravian tanzania kuanzia wilaya,jimbo kuwa na ofisi za kisasa lengo likiwa ni kusogeza huduma za kiroho kwa waumini wake.
na Hobokela Lwinga
Makamu Mwenyekiti wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Mch. Asulumenye Mwahalende amezindua ofisi kuu za wilaya ya Mbalizi zenye lengo la kutoa huduma za kiroho kwa waumini na shirika za wilaya hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Makamu Mwenyekiti huyo amewataka Wakristo kuzitumia ofisi hizo kwa lengo lililokusudiwa la kuratibu shughuli za kiroho kwa ustawi wa kanisa la Mungu.
Aidha akihubiri katika ibada hiyo Mchungaji Mwahalende amewataka Wakristo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kwa kujiandikisha na kupiga kura.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kanisa la Moravian wilaya ya Mbalizi Mch.Elika Mwanijembe amesema wilaya yake inatarajiwa kujenga vitega uchumi vingine ikiwemo shule na ukumbi mkubwa sambamba na uzalishaji wa zao la parachichi.
Baadhi ya waumini katika wilaya hiyo wamefurahishwa na uwepo wa ofisi hizo huku wakiushukuru uongozi wao kusimamia vyema na kufanikisha ujenzi huo.