Askofu Pangani atoa ujumbe mzigo kwa kanisa na Taifa juu ya matukio ya utekaji na mauaji
23 September 2024, 17:24
Kutokana na hali ilivyo nchini ya matukio ya watu kutekwa na kuuawa imemlazimu askofu Pangani kutoa kauli ya kukemea matukio hayo.
Na Ezekiel Kamanga
Askofu Robert Pangani wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi amewataka Waumini na Watanzania kwa ujumla kuiombea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuendelea kudumisha amani nchini.
Askofu Robert Pangani ametoa wito huo katika ibada maalumu ya mbaraka kwa Mashemasi kumi na sita na Makasisi watatu ibada iliyofanyika Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Nzovwe kiongozi wa ibada akiwa ni makamu Mwenyekiti wa Jimbo Mchungaji Asulumenye Dickson Eva Mwahalende.
Amesema hafurahishwi na vitendo vya utekaji na mauaji ya watu yanayoendelea nchini hivyo ameziomba Mamlaka husika kuwabainisha watu hao kuendelea kudumisha amani nchini sanjari na kuondoa hofu kwa wananchi.
Aidha Pangani amewataka Mashemasi na Makasisi katika ofisi zao kuwa faraja badala ya kuwa na makwazo kwa waumini wanaowaongoza.
Amewaonya Wachungaji kusimamia na kutunza fedha za Kanisa Ili zifanye kazi kama ilivyokusudiwa na Wachungaji wanaotarajia kujinufaisha kupitia madhabahu hawana nafasi wakifanya kazi kwa uadilifu watapata baraka.
Katika hatua nyingine amewataka viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Taifa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwani wananchi wengi wana kero lakini hazitatuliwi kwa wakati.
Amehitimisha Mahundi yake kwa kuwataka Wakristo kujiepusha na Wachungaji,Manabii na Mitume ambao hulitumia neno la Mungu kuwatapeli watu.