Baraka FM

Watuhumiwa 992 wakamatwa kwa tuhuma mbalimbali Mbeya mwezi agosti,2024

4 September 2024, 17:32

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi [SACP] Benjamin Kuzaga

Katika kipindi cha mwezi Agosti , 2024 jumla ya watuhumiwa 992 wa makosa mbalimbali yakiwemo makosa ya mauaji, kujeruhi, wizi pamoja na kupatikana na nyara za serikali.

Na Hobokela Lwinga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuimarisha ulinzi na Usalama wa raia na Mali zao kwa kufanya doria na misako pamoja na kutoa elimu ya Polisi Jamii hali ambayo imepelekea kupata mafanikio katika kuzuia na kupambana na uhalifu.

Akizungumza na wananchi kupitia Mkutano wa waandishi wa habari Septemba 04, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi [SACP] Benjamin Kuzaga ameeleza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Jema Majolini [43], Mkazi wa Godauni Chalisuka kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali vipande kumi na mbili vya nyamapori ya mnyama Nyati iliyokaushwa.

Mtuhumiwa alikamatwa na nyari hizo akiwa ameficha ndani ya chumba chake anachoishi kwa lengo la kuiuza. Wakati huo huo Jeshi la Polisi Mkoa wa linawasaka watuhumiwa watatu ambao wanatambulika kwa sura baada ya kukimbia na kutekeleza pikipiki na nyara serikali jino moja la Tembo lenye uzito wa kilogramu Saba, jino la Ngiri na nyama ya ngiri ambavyo walikuwa wameficha kwenye mfuko wa Sandarusi na kupakia kwenye Pikipiki MC 967 ELK aina ya TVS. Watuhumiwa ni wawindaji haramu katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Vile vile katika mapambano dhidi ya wizi wa vyombo vya moto aina ya pikipiki Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu Rafael Edward [30], mkazi wa Lyambogo, Juma Ibrahimu [26] mkazi wa Mwale na Yusufu Wihanji [ 35], mkazi wa Mwale kwa tuhuma za wizi wa Pikipiki sita ambazo waliiba katika maeneo tofauti ya Mkoa wa Mbeya.

Pikipiki zilizokamatwa ni MC 139 CNX aina ya SanLg, MC 488 BSJ aina ya SanLg, MC 263 DFM aina ya SanLg, MC 314 ASP aina ya Kinglion pamoja na Pikipiki mbili zisizo kuwa na namba za usajili aina ya Kinglion ambazo ni Mali za wizi .Pikipiki hizo zilikutwa zimefichwa nyumbani kwa Mtuhumiwa Yusufu Wihanji, mkazi wa Mwale Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.

Watuhumiwa wamekiri kuhusika katika matukio ya uporaji na wizi wa Pikipiki katika maeneo tofauti Wilayani Mbarali . Watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.